Tuesday, April 23, 2024
Home > Counties > Elgeyo Marakwet > Gavana afanya mabadiliko ya baraza lake

Gavana afanya mabadiliko ya baraza lake

Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Alex Tolgos amefanya mabadiliko katika baraza lake la wanakamati kuu wiki moja tu baada ya kuwapa maafisa wote wakuu likizo ya lazima.
Mwanakamati mkuu anayesimamia kilimo na unyunyizaji maji Shadrack Yatich amehamishwa hadi idara ya utalii, uchumi, viwanda na wanyama pori huku nafasi yake ikichukuliwa na mwenzake aliyekuwa anasimamia utalii bi. Ann Kibosia.
Gavana huyo pia amempa likizo ya lazima afisa anayesimamia ununuzi Robert Chelagat aliyeagizwa kumuachia naibu wake afisi.
Tolgos alisema amechukua hatua hiyo kama hatua moja ya kuimarisha utendakazi katika serikali yake huku akiwasuta wanakamati kuu dhidi ya kuzembea kazini akisema hatasita kuwachukulia hatua.
Yatich na Kibosia ndio wanakamati kuu ambao waliendelea kushikilia nyadhifa zao huku wengine wote wakiwachishwa kazi baada ya gavana kushinda kwa kipindi chake cha pili.
Gavana huyo alisema nia yake ni kuhakikisha kwamba wakaazi wanapata huduma za hali ya juu ili kuwezesha kaunti hiyo kupata maendeleo.
By Alice Wanjiru

Leave a Reply