Thursday, October 3, 2024
Home > Counties > Elgeyo Marakwet > Kijana 24, afungwa maisha

Kijana 24, afungwa maisha

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 24 amefungwa maisha na mahakama moja mjini Iten baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa miaka 7.
Hakimu mkuu mwandamizi Hezron Nyaberi alimpata Joshua Kemboi na hatia ya kumnajisi mtoto huyo mnamo tarehe 5 Februari 2017 mwendo wa saa saba unusu katika kata ya Kiptuilong kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Nyanyake mtoto huyo ambaye amekuwa akiishi naye aliielezea mahakama kwamba alikuwa amemwacha mjukuu wake akicheza na wenzake na kuelekea malishoni.
Aliporudi alimpata akilia huku akichechemea kwa uchungu na alipomuuliza yaliyojiri, akamweleza jinsi mshukiwa alivyomchukua chumbani kwake na kumnajisi.
Nyanyake aliiambia mahakama alimpeleka katika hospitali ya Tambach ambapo daktari alidhibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa amenajisiwa.
Aliendelea kusema alienda na mjukuu wake hadi kituo cha biashara ambapo mtoto huyo aliweza kumtambua mshukiwa licha ya kuwa ana nduguye ambaye wanafanana.
Mshukiwa alijipata matatani alipoiambia mahakama kuwa ingawa alikuwa ameishi mahali pale kwa muda wa miaka kumi, hakumjua mlalamishi wala nyanyake.
Hata hivyo, babake John Cherutich ambaye ni mhubiri alisema mwanawe anaidanganya mahakama kwani mlalamishi na nyanyake wanaishi takribani mita 200 kutoka kwa nyumba yake.
Akijitetea, mshukiwa aliitaka mahakama imsamehe akisema kwamba bado yeye ni kijana mdogo na anaugua ugonjwa wa homa ya mapafu.
Ikitoa hukumu, mahakama ilisema imetosheka na ushahidi uliotolewa hasa na mlalamishi huku ikisema ushahidi huo ulidhibitishwa na daktari kwamba mtoto huyo alikuwa amenajisiwa.
Mahakama iliongeza kwamba kadi ya hospitali ilionyesha mlalamishi alizaliwa Agosti 5 2010 na hivyo basi alikuwa na umri wa miaka 7 aliponajisiwa.
Mahakama ilisema imezingatia malilio ya mshukiwa lakini kulingana na sheria na kosa alilotenda hawezi kuepuka kifungo cha ndani na hivyo basi kupewa kifungo cha maisha.
Mshukiwa ana siku 14 kukata rufaa.
By Alice Wanjiru

Leave a Reply