Tuesday, December 10, 2024
Home > Counties > Viongozi wa Pwani waghadhabishwa na ongezeko la  mimba kwa wasichana wa shule

Viongozi wa Pwani waghadhabishwa na ongezeko la  mimba kwa wasichana wa shule

Viongozi mbali mbali katika Kaunti ya Pwani wamelaani ongezeko la visa vya kutungwa mimba wasichana wa shule na wale hawajakomaa.

Viongozi hao walishtumu vitendo vya kutia mimba watoto wa shule wakihoji kwamba mbali na kuwa ni kero tabia hiyo  imerudisha nyuma pakubwa manufaa yaliyopatikana ya kuelimisha mtoto msichana.

Wakati wa mahojiano na shirika la habari inchini (KNA), baadhi ya viongozi hasa  kutoka kaunti ya Kilifi ambako visa vingi vya wasichana wadogo kupachikwa mimba vimeripotiwa, waliwakashifu walimu wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi wakike badala ya kuwafunza maadili mema.

Aidha walikilaumu chama cha walimu (KNUT) kwa kukosa kulizungumizia swala hili kwa uzito kama vile wanavyofanya wakati wa kupigania nyongeza za mishahara ya wanachama wao na maslahi mengineyo.

Kaunti za Kilifi na Kwale zinasadikika kuwa miongoni mwa maeneo yanayongoza kwa visa vya kutungwa mimba kwa wasichana wa shule na ndoa za mapema.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana amesema ni muhimu hatua za haraka kuchuliwa ili kukomesha tabia hiyo ambayo aliitaja kama dhuluma  kwa  wasichana wadogo.

“Serikali kuu na viongozi wote lazima watafute njia muafaka ya kukomesha tabia hii mbofu  ambayo imeharibu maisha ya wasichana wadogo na pia kuleta aibu kubwa kwa jamii,” alisema Katana.

Mbunge huyo kutoka kaunti ya Kilifi alisema ni lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya wale wenye ‘uchu’ kwa wasichana wa shule na wale wenye umri mdogo.

Mshindi wa tuzo la utalii katika kaunti ya Kilifi mwaka huu (2018) Christine Majeni alieleza masikitiko yake juu ya ongezeko la visa vya utiaji mimba wasichana wa shule katika sehemu hiyo.

Yaniuma sana kuona kaunti yetu inaongoza katika visa vya kutiwa mimba kwa wasichana wa shule na ndoa za mapema,” alisema Majeni.

Kadhalika Bi Majeni alisema ni lazima viongozi wote, wazazi na washikadau katika sekta ya elimu  kwenye kaunti ya Kilifi kukaa chini na kutafuta suluhisho la kudumu la kumaliza udhia huu.

Alisema ni kupitia tu njia ya elimu wasichana wataweza kusaidiwa kukuza vipaji vyao ili waweze kutekeleza majukumu muhimu katika jamii na pia kuboresha maisha yao.

Hisia hizi kali zinaibuka baada ya kubainika kuwa wanafunzi wengi humu nchini walilazimika kufanya mitihani yao ya darasa la nane na kidato cha nne wakiwa wamejifungua na wengine wakiwa na mimba.

Ni jambo ambalo limezua tumbo joto na kusababisha mjadala mkali hasa katika mitandao ya kijamii ambapo wakenya wengi walisema hili ni ‘janga la kitaifa’ na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa.

Waziri wa elimu  Bi Amina Mohamed alitaja visa hivi kama unyama dhidi ya wasichana wachanga na akasema serikali iko katika harakati za kuunda mbinu za kuliangamiza jinamizi hili.

“Inasikitisha kuona wale ambao wamepewa jukumu la kuwatunza watoto wa shule ndio wanaowafanyia dhuluma na kuwaharibia maisha yao,” alisema Waziri Mohamed.

Akiongea wakati wa siku ya kwanza ya mtihani wa kidato cha nne mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Waziri Amina alisema wakati umefika kwa wakenya kulizungumzia janga hili kwa kina na kutafuta suluhisho la kudumu.

“Wale wanaohusika na utungaji mimba wa wasichana wa shule ni sawa na wabakaji na lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria,” alisema waziri huyo.

Mwanachama wa shirikia la kupambana na mihadharati humu nchini (NACADA) Farida Rashid pia alilaani vitendo vya kuwaharibia maisha wasichana wadogo.

Alisema wale wote wanaohusika wakiwemo walimu ni lazima wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo ambayo alisema inaenda kinyume na maadili mema.

Pia Bi Rashid alihusisha vitendo hivyo vya kutiwa mimba kwa wasichana wadogo na utimiaji wa mihadharati.

“Ni wazi wengi wanaojihusisha na kuwadhulumu wasichana wadogo huwa waraibu wa mihadarati. Mtu mwenye akili timamu hawezi kulala na msichana wa shule au mwenye umri mdogo,” aliongeza kusema mwanachama huyo wa NACADA.

Alitilia mkazo hoja kuwa ni muhimu kwa bunge la taifa kulijadili jambo hilo kwa haraka na kutunga sheria kali dhidi ya wale wanaodhalilisha wasichana wadogo.

Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga ameitaka serikali kupiga marufuku dansi za usiku za matanga (disco matanga) katika kaunti ya Kilifi ambazo alisema zimechangia pakubwa kutungwa mimba kwa wasichana wa shule na wale wenye umri mdogo.

“Sherehe hizi za usiku hazina maana yoyote na zimechangia sana kudorora kwa viwango vya elimu, ukosefu wa nidhamu na  ongezeko la visa vya mimba miongoni mwa wasichana wadogo,” alisema Chonga.

Mbunge huyo alilaani kuweko kwa dansi hizo katika sehemu hiyo ambazo alisema ndizo chanzo kikubwa cha mimba za mapema na kuolewa kwa wasichana wakiwa na umri mdogo.

Alisema sherehe hizo ambazo hutumiwa kuchangia fedha  kusaidia gharama za matanga ni potofu na zimechangia kudorora tabia kwa vijana.

 

Na Mohamed Hassan

Leave a Reply