Wednesday, December 4, 2024
Home > Counties > Vita dhidi ya dawa za kusisimua misuli vyaimarishwa

Vita dhidi ya dawa za kusisimua misuli vyaimarishwa

Mwanariadha yeyote atakayepatikana akitumia dawa za kusisimua misuli atapigwa marufuku kuwakilisha nchi ya Kenya katika mashindano yoyote ya mbio.

Hii ni baadhi ya mikakati ambayo imewekwa na shirika la Anti-Doping Agency of Kenya (ADAK) kukabiliana na changamoto hii ambayo inatishia kuharibu sifa ambazo nchi hii imepata ulimwenguni kote kutokana na umahiri wake katika riadha.

Rais wa shirika la Athletics Kenya (AK) generali mstaafu Jackson Tuwei aliendelea kusema mwanariadha ambaye ni mfanyi kazi wa serikali atafutwa kazi kabla ya kufikishwa mahakamani iwapo atapatikana akitumia dawa hizo.

Kutoka kushoto wanariadha Edna Kiplagat, David Rudisha na gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Alex Tolgos waliposhiriki katika kampeini dhidi ya dawa za kusisimua misuli.

Tuwei alikuwa akizungumza mjini Iten wakati shirika la ADAK lilipoandaa mkutano wa siku moja katika uwanja wa michezo wa Iten kuwahamasisha wanariadha kuhusu hatari za kutumia dawa za kusisimua misuli.

Rais huyo alisema wanashirikiana na wizara ya elimu kuwasajili wanariadha wachanga katika shule za msingi katika juhudi za kukusanya data ya wakimbiaji wote kuzuia visa vya undanganyifu.

“Tumegundua kwamba kuna wanariadha ambao wakishapigwa marufuku baada ya kupatikana na makosa huwa wanabadilisha jina lao na kuendelea kukimbia, tukiwa na data kuwahusu tutazuia visa kama hivi,” alisema Tuwei.

Mkurugenzi mkuu wa ADAK Japhet Rugut aliwataka mashirika ya wanariadha, meneja na makocha kushirikiana na ADAK katika juhudi za kutatua tatizo la matumizi ya dawa hizo ambayo alisema yanadhuru wanariadha kiafya.

“Mameneja na makocha huwa na wariadha kila siku na kwa hivyo wanawajua na watajua ikiwa watatumia dawa hizo,” alisema Rugut.

Rugut alisema wanariadha watakuwa wakipimwa kila baada ya miezi sita na kabla ya kushiriki kwa mbio zozote akiongeza kuwa wanaangalia pia wanavyokimbia na ikiwa mwanariadha anakimbia vizuri ghafla halafu anadidimia watajua anatumia dawa za kusisimua misuli.

Wanariadha watajika kama David Rudisha, Wilson Kipsang na Mary Keitany walihudhuria hafla hiyo na kuwasihi wanariadha chipukizi dhidi ya kujiingiza katika uovu huo.

Kipsang pia aliitaka serikali kuu na ile ya kaunti kukamilisha uwanja wa Kamariny na kukarabati viwanja vingine ili kutoa nafasi ya wanariadha kufanya mazoezi.

“Uwanja wa Kamariny umechukua muda mrefu kabla ya kukamilika jambo ambalo limeathiri mazoezi kwa wanariadha wengi hasa wale ambao hawawezi kumudu nauli ya kusafiri hadi Eldoret kufanya mazoezi,” alisema Kipsang.

Na Alice Wanjiru

Leave a Reply