Mgombea kiti cha mwakilishi wa wadi (MCA) cha Narok Town kupitia chama cha Democratic Citizens Party (DCP), Douglas Masikonde ametangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi mdogo uliokamilika jana.
Masikonde alimshinda Kayinke Ole Kudate wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa kura 1,518 pale alipojinyakulia kura 5,997.
Ukumbi wa shule ya upili ya wasichana ya Maasai ulijawa na furaha riboribo pale tangazo hili lilifanywa na msimamizi wa uchaguzi wa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya IEBC, Mbugua Kuria.
Akiwahutubia wakaazi muda mchache baada ya kutangazwa mshindi, Douglas Masikonde aliwashukuru wapiga kura na kusema yuko tayari kuwafanyia kazi akisema kuwa atashirikiana hata na viongozi wengine ili kuona kwamba wadi ya Narok town inaendelea.
Masikonde aliwaomba wakaazi pamoja na wapinzani wake kuweka tofauti zao za kisiasa kando ili waweze kuwa na mwelekeo mwema katika utendakazi wao.
Aliyemfuata kwa nafasi ya pili alikuwa Kudate ambaye pia ni mtoto wa aliyekuwa mwakilishi wa wadi wa eneo hili, marehemu Lucas Ole Kudate kwa kupata kura 4,479 huku wagombea wengine wakijinyakulia kura chini ya 100 Kila mmoja.
Hapo jana, wagombea wengine walitoa malalamishi ya wapiga kura kuhongwa huku Masikonde akifurushwa kutoka kituo cha kupiga kura cha shule ya msingi ya Masikonde muda mchache baada ya kupiga kura na baadhi ya wafuasi wa wapinzani wake.
Hali hii ilizua vurugu lakini maafisa wa usalama walisalia ange na kuidhibiti hali hii na kuona kuwa shughuli ya kupiga kura inakamilika kwa wakati ufaao.
Kuria alimpongeza Masikonde kwa ushindi alioupata huku akionyesha kuwa wadi hii inawapiga kura 29,452. Kati Yao, ni 10,700 pekee waliompiga kura huku kura 116 zikikataliwa.
Na Emily Kadzo
