Familia moja katika eneo la Ntulele, Narok Mashariki, wanawaomba wahisani kujitokeza na kumsaidia mtoto wao kuweza kuhifadhi nafasi yake ya gredi ya 10 katika shule ya sekondari ya juu ya St. Joseph iliyoko katika gatuzi la Nyeri.
Liten Limpaka alipata fursa ya kujiunga na shule hii baada ya kuzoa alama 51 katika mtihani wa Kitaifa wa KJSEA hapo mwaka jana.
Hata hivyo, Limpaka alieleza kwamba familia yake imekumbwa na changamoto kuu ya ukosefu wa fedha kiasi cha kwamba analazimika kutafuta vibarua kuona iwapo ataweza kuweka akiba ya kupata karo ya shule.
“Nina mzazi mmoja ambaye ni mama yangu. Yeye huugua mara kwa mara na hivyo basi inanibidi nijikaze na kuwashughulikia ndugu zangu wengine watano ili angalau waweze kupata chakula kila siku,” alisema Limpaka.
Kutokana na hili, alisema kuwa yeye hutafuta vibarua kama vile kulisha mifugo, kulimia watu katika mashamba yao ambapo analipwa kati ya shilingi 200 hadi 250 kwa siku; ambazo hazitoshi kamwe kwani kuna wakati inambidi asubiri malipo au anakosa kibarua cha siku.
Ama kweli, jirani yao ambaye pia ni mhamasishaji wa afya ya jamii katika kituo cha afya cha Ntulele, Bi. Elizabeth Njeri, alisema kuwa familia hii imepitia changamoto si haba na kama majirani wamewasaidia vilivyo kuona kwamba wanayaimarisha maisha yao.
“Kama jamii, tumesaidia familia hii kupata chakula, mavazi na hata mahala pa kuishi kwa kuwajengea nyumba kwa kuwa mama yao hajiwezi kamwe. Tunaomba wahisani wamsaidie Limpaka kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanajeshi pindi atakapoyakamilisha masomo yake, ” aliomba Bi. Njeri.
Mkurugenzi wa shirika la Enetoto Oloshoo ambaye pia ni jirani yao, Bi. Jemimah Torome kwa upande wake alisema kuwa walichukua jukumu la kumsomesha Limpaka kwa kumlipia karo ya shule, kumnunulia vitabu na mahitaji yote ya shule tangu alipokuwa gredi ya sita hadi tisa. Aliwaomba wahisani kuinua familia hii kwa kumsomesha kijana huyu ili apate fursa ya kuyageuza maisha ya familia yao katika siku za usoni.
Mzee wa Kijiji wa eneo hili, Bw. Jackson Obiki alisema masomo yanasalia kuwa kiungo muhimu katika maisha ya sasa na hivyo basi inabidi wahusika wote ikiwemo viongozi wasaidiane katika kuwapeleka watoto wanaopitia changamoto za aina hii shuleni ili waweze kuendeleza nchi katika nyanja mbalimbali.
Takwimu kutoka wizara ya elimi zinaonyesha kuwa ni wanafunzi takriban 800,000 ambao hawajaripoti katika shule za upili za juu kutokana na shida kadha wa kadha wanazokumbana nazo na Limpaka anasalia kuwa katika orodha hii.
Hatma yake Limpaka imesalia mikononi mwa wahisani na ana matumaini ya kujiunga na shule ya sekondari ya juu siku moja.
Na Emily Kadzo
