Wednesday, February 11, 2026
Home > Counties > Kamishna awahimiza wafanyikazi wa serikali kukumbatia mfumo wa BETA

Kamishna awahimiza wafanyikazi wa serikali kukumbatia mfumo wa BETA

Kaunti Kamishna wa Narok, Kipkech Lotiatia amewahimiza watumishi wote wa umma kukumbatia ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi Chini ya BETA kwa lengo la kusaidia kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo ya siku mbili kwa wakurugenzi wa kaunti kutoka Idara mbalimbali ikiwemo wakuu wa tarafa (ACC) na wadoga wa kaunti kamishna  (DCC), Kipkech alisema kuwa kwa kufanya hivyo, itaharakisha mchakato wa utekelezaji BETA na kupata fursa ya utawala bora.

‘’Rais William Ruto anautumia mfumo huu kuimarisha maisha ya wakenya na ni wajibu wetu kama wafanyikazi wa serikali kumuunga mkono kwa kuzingatia nguzo hizi tano muhimu,’’ alieleza Kamishna.

Nguzo hizi zinazotumika kwa minajili ya kupunguza gharama ya maisha, kutokomeza njaa, kuunda ajira na kupanua wigo wa kodi ni kama vile mageuzi ya kilimo ili kuimarisha uzalishaji wa chakula, Uchumi wa MSMEs unaosaidia biashara ndogo na za kati, afya inayo boresha huduma za afya (Universal Health Coverage), nyumba na makaazi kwa kujenga nyumba nafuu pamoja na uchumi wa kidigitali unaokuza teknologia na ubunifu.

‘’Ili kuafikia lengo hili, kuna haja ya ushirikiano mkuu katika idara mbalimbali bila kujali changamoto zinazojitokeza,’’ alisema Kipkech.

Hata hivyo, aliwaomba wakurugenzi kutochangia katika kueneza uvumi kuhusu mpango huu bali wawe mabalozi wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kwa kuwa itasaidia serikali kufanikiwa katika juhudi zake za kuinua maisha ya watu.

Mafunzo haya yaliongozwa na Afisi ya rais kupitia wafanyikazi wa kitengo cha utoaji huduma cha serikali yaani Government Delivery Unit.

Na Emily Kadzo

 

Leave a Reply