Mama mmoja wa umri wa makamo alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na fisi katika eneo la Rimoi katika kaunti ndogo ya Keiyo Kaskazini.
Mama huyo, Hellen Chepsergon, ambaye anaendelea kuuguza majeraha katika hospitali ya rufaa ya Iten alivamiwa mwendo wa saa kumi na moja jioni hapo jana alipokuwa anatoa mifugo wake malishoni.
Bi. Chesergon aliumizwa sehemu mbali mbali mwilini na kupoteza kidole chake kimoja huku madaktari wakisema lazima kingekatwa kwani kilikuwa kimeumizwa sana kupitia machambulizi mnyama huo.
Dkt. Lawrence Kogos alisema madaktari wailmhudumia kwa haraka pindi tu alipofikishwa hospitalini akisema yuko katika hali nzuri ingawa alipata majeraha ya kudumu ambayo yataadhiri maisha yake ya baadaye.
Dkt. Kogos alisema baada ya matibabu, hospitali hiyo itatoa ushauri nasaha kwa mama huyo ili kuweza kukabiliana na mshtuko aliopata kutokana na tukio hilo.
Kijana mmoja kwa jina Ian Kipkorir pia alifikishwa katika hospitali hiyo hiyo akiwa na majeraha ya mkononi baada ya kuumizwa na fisi huyo alipokuwa anamwokoa mama huyo.
Kipkorir alisema alikuwa nyumbani aliposikia mama akipiga mayoe na mara hiyo hiyo akachukua panga na kuelekea mahali sauti ilikuwa inatoka.
“Nilifika hapo na kumkuta mama huyu aking’ang’ana na huyo fisi na baada ya kuniona fisi huyo aliwachana na mama na kunivamia na akaniuma mkono,” alisema Kipkorir.
Akisimulia kisa hicho hospitalini, kijana huyo alisema aliweza kumkata kichwa na kumuua yule mnyama na kuokoa maisha ya Mama Hellen ambapo majirani walifika na kuwakimbiza kwa hospitali.
Afisa anayesimamia idara ya huduma ya wanyama pori katika kaunti Nelson Cheruiyot alisema idara hiyo itafuatilia kuona kuwa wawili hao wamefidiwa kutokana na majeraha waliopata.
Cheruiyot alisema huenda fisi huyo alikuwa anatafuta chakula kwani alikuwa ametoka katika mbuga la wanyama la Rimoi na kwenda katika makazi ya wananchi.
Mbunge wa eneo hilo Adams Kipsanai alisema walikuwa wametenga fedha za kuweka ua katika mbuga hiyo ili kuzuia visa kama hivyo akisema watafuatilia na wizara ya utalii kuona kwamba fedha hizo zimetolewa na ua kujengwa.
Na Alice Wanjiru
