Wakaazi wa eneo la Narok Kusini wameapa kuendelea na juhudi za upanzi wa miti katika msitu wa Maasai Mau ili kusaidia kurejesha misitu katika maeneo yaliyotambuliwa kama vyanzo vya maji.
Wakizungumza wakati walipokuwa wakiirudishia shukrani kampuni ya Base Titanium kwa kuwapa mafunzo ya ulezi wa miti na kilimo cha nyuki, chama cha mazingira cha Kirobon (CBO) kilicho na wanachama mia moja, walisema wametambua manufaa makubwa ya utunzi wa miti kwani wanauwezo wa kupata riziki na kulea familia zao huku misitu ikiendelea kunawiri.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama hicho, Wycliffe Kimutai, alisema kuwa kufurushwa kwao katika msitu wa Maasai Mau kulizima ndoto zao za maisha wasijue watakapoanzia upya.
Waliiona hali hii kama dhiki lakini tangu mwaka wa 2019 ambapo walianza kupokea mafunzo kutoka kwa kampuni ya Base Titanium, wanaona kuwa wanaendelea kubadilisha maisha yao.
Kama kikundi, wamepokea mafunzo ya kukuza na kulea miche ambayo wanaiuza na kupata faida.
“Kampuni ya Base Titanium ni mojawapo wa wateja wetu wakuu kwani wametununulia zaidi ya miche 50,000,” alisema Kimutai.
Mwanachama Karen Chepkoech, naye kwa upande wake alisema, mafunzo haya yamemuezesha kukaa mbali na hali zinazoweza mvutia kuingia katika uhalifu kwani hata wale wanaoipanda miche ile wanalipwa na kutokana na riziki, wanaweza kushughulikia mahitaji yao.
“Katika kikundi hiki, walio wengi ni vijana na hivyo basi kutokana na malipo wanayoyapata kupitia ukuzaji wa miche, wameasi mienendo potovu na kufanya kazi inayowapa hadhi ya juu katika jamii,” alinena Chepkoech.
Mbali na ukuzaji wa miche, wanachama hawa waliweza kupokea vifaa vya kisasa vya kuwawezesha kufanya kilimo cha nyuki na kufikia sasa, wanauwezo wa kupokea hadi kilo 80 za asali wanayoiunda na kuiuza.
Kwa upande wa Joshua Koech aliyetoka msituni baada ya serikali kutoa agizo hilo, anasema kuwa ameona tofauti kubwa na misitu imeendelea kunawiri hasa maeneo yaliyokuwa yameathirika sana.
Aliomba mashirika mengine kuiga mfano wa Base Titanium na juhudi za kuimarisha misitu ili kufanikisha azma ya Rais ya upanzi wa miti bilioni 10.
Wanachama hawa waliweza kusema ya kwamba shughuli hizi zinazowasaidia kupata mapato zitawasaidia kukuza upendo wa upandaji wa miti katika watoto wao na hata vizazi vijavyo.
Base Titanium ni kampuni inayochimba madini kutoka mgodi katika gatuzi la Kwale.
Na Emily Kadzo
