Monday, January 26, 2026
Home > Counties > Epukeni mihadarati ili mtimize malengo yenu maishani, wanafunzi washauriwa

Epukeni mihadarati ili mtimize malengo yenu maishani, wanafunzi washauriwa

Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Narok Rebecca Tonkei amewataka wanafunzi kuepuka matumizi ya madawa ya kulevya ili kutumia fursa yao shuleni vyema kuinua hali yao ya maisha.

Akizungumza katika Shule ya Bweni ya Olesankale mjini Narok, Bi Tonkei, ambaye pia aliwahi kuhitimu kama Mwalimu, alisema hayo wakati wa kuzindua mpango wa kufadhili masomo ya wanafunzi wa kike walio na nidhamu ya hali ya juu na watakaopata matokeo bora katika mitihani yao.

Alisema kuwa vijana wengi walioingililia uraibu wa madawa ya kulevya na pombe hupata kwamba wamekatiza malengo yao katika siku za usoni na wengine kujipata wameyapoteza maisha yao katika umri mdogo.

Kwa mujibu wa Bi. Tonkei, ni hali inayosikitisha sana na ni vyema kuwa na ushirikiano kuona kwamba vijana wanasalia shuleni na wale walioingililia uraibu huu kupata kurekebishwa mapema ili wote wapate fursa ya kubadilisha maisha yao kuwa bora.

Aliwashauri wanafunzi pamoja na wazazi waliokuwepo katika hafla hio kutafuta ushauri nasaha kwani ni jambo ambalo pia husambaratisha familia nyingi.

Kaunti ya Narok ilikuwa na idadi ya asilimia 42.33 ya wanafunzi wa kike katika shule za upili ikilinganisha na wanafunzi wa kiume waliokuwa asilimia 57.67 katika mtihani wa Kitaifa wa KCSE mwaka jana; huku wale wanaofuzu kwenda vyuo vikuu ikiwa chini zaidi.

Bi Tonkei alisema masomo ni muhimu katika kuchangia ubora wa viongozi akisema wasomi huonyesha uongozi bora kwani wanaelewa dunia ilivyo sasa.

Kulingana na takwimu za mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, Narok ni moja yapo ya kaunti kumi zilizo na wavulana wengi kuliko kina dada waliofanya mtihani huo.

 na Emily Kadzo

Leave a Reply