Saturday, February 14, 2026
Home > Counties > Mau Mau Original Trust yalalamikia kundi bandia

Mau Mau Original Trust yalalamikia kundi bandia

Naibu mwenyekiti wa Mau Mau Original Trust nchini, Daniel Mwangi, ameisihi Serikali kulichukulia hatua kundi analodai kuwa ni bandia linalotumia jina la asasi hiyo kuendesha shughuli zake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Narok, Mwangi alisema kuna haja kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kundi hilo, akidai kuwa limekuwa likiwahadaa wanachama na kujinufaisha kwa misingi isiyo halali.

Mwangi alieleza kuwa baadhi ya viongozi wa kundi hilo wamefika hadi Ikulu ya Rais wakijitambulisha kama wawakilishi halali wa wanachama wa Mau Mau Original Trust, jambo alilolitaja kuwa la kupotosha na linaloweza kuvuruga juhudi za wanachama halisi.

“Kama uongozi halali wa Mau Mau Original Trust, tunapinga vikali vitendo vya kikundi hiki. Serikali inapaswa kuingilia kati haraka iwezekanavyo ili kulinda heshima na uhalali wa asasi yetu,” alisema Mwangi.

Alionya kuwa iwapo kundi hilo litaendelea na shughuli zake, linaweza kuvuruga mipango na shughuli rasmi za wanachama halali, akisisitiza kuwa nia ya wanaojiita viongozi wa kundi hilo ni kujinufaisha kibinafsi.

Kwa sasa, Mwangi alisema kuwa asasi yao inaendelea kuwahusisha wanachama wake kote nchini waliopigania uhuru wa taifa ili kuweka mikakati ya pamoja kuhusu suala la fidia. Alisema mchakato huo unafanywa kwa uwazi na ushirikishwaji wa wanachama wote bila ubaguzi wowote.

Aidha, aliwahakikishia wanachama kuwa hakuna atakayeachwa nje katika juhudi hizo na kwamba zoezi linaendeshwa bila malipo yoyote.

“Tunataka wanachama wetu wawe na imani kuwa hakuna malipo yanayohitajika kushiriki katika mikutano au michakato yetu. Hatutambui ada yoyote wala mchango wa lazima,” alisisitiza.

Mwangi aliomba Serikali kuendelea kushirikiana na uongozi halali wa Mau Mau Original Trust ili kuhakikisha kuwa masuala yanayohusu wanachama, hususan madai ya fidia, yanashughulikiwa kwa njia sahihi na ya haki.

Alimalizia kwa kusisitiza umuhimu wa kulinda historia na heshima ya wapigania uhuru, akisema kuwa ni jukumu la kila mdau kuhakikisha kuwa majina na juhudi zao hazitumiki vibaya kwa maslahi binafsi.

Na Emily Kadzo

Leave a Reply