Kaimu kamishina wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Julius Maiyo amewaonya watu wanaochochea vurugu kati ya wananchi katika eneo la Kamoingon kaunti ndogo ya Keiyo Kaskazini kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hili linafuatia tukio ambapo watu wawili walijeruhiwa kwa mishale huku mmoja akikatwa kwa panga kutokana na mzozo wa ardhi katika eneo hilo ambapo zoezi la upimaji mashamba linaendelea.
Aliongeza kuwa nyumba kumi na mmoja ziliteketezwa na kuwaacha wakazi bila makao katika tukio hilo lililotokea mwisho wa wiki jana.
Maiyo alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea akiongeza kwamba polisi walipata majina ya watu ambao wanatuhumiwa kuchochea mzozo huo.
Maiyo alitoa wito kwa wakazi kuwa watulivu hadi pale zoezi la upimaji wa mashamba litakapokamilika akisema zoezi hilo litaweza kubaini ni nani anayemiliki vipande mbali mbali vya ardhi katika eneo hilo.
Kamishina huyo alisema serikali imeweka mikakati ya kutosha ikiwemo kuwatuma polisi wa kutosha kushika doria katika eneo hilo ili kurejesha hali ya utulivu.
Aliwasuta wakazi dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao akisema kuwa machifu na vingozi wa nyumba kumi wanafuatilia ili kuona kuwa kuna amani ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Na Alice Wanjiru
