Wednesday, October 4, 2023
Home > Counties > Bungoma > Bungoma yang’aa kwenye mashindano ya shule za upili 

Bungoma yang’aa kwenye mashindano ya shule za upili 

Michezo ya shule za upili ngazi ya kitaifa inajongea kidedea huku jimbo la Bungoma likijivunia takriban shule tatu zilizofuzu kuliwakilisha jimbo hilo katika kanda ya Afrika Mashariki.

Awali jimbo hilo lilitoa takriban shule tano kuwakilisha kanda ya magharibi katika kipute hicho zikiwemo shule ya wavulana ya Kamusinga ikiwakilisha katika mchezo wa magongo, ile ya wavulana ya Namwela kwenye voliboli, ile ya Bukembe iliyobanduliwa kwenye soka na kamati ya michezo ya shule za upili, shule ya upili ya Mtakatifu Cecilia Misikhu na ile ya wasichana ya Kamusinga.

Akizungumza na KNA jumapili jioni, katibu mkuu wa shirikisho la michezo ya shule za upili Kenya Secondary Schools Association (KSSSA) David Ngugi alivipongeza vikosi vitatu kwa kufuzu kuwakilisha taifa la Kenya kwenye ukanda wa Afrika Mashariki vyote vikitokea kaunti ya Bungoma.

“Niwapongeza pakubwa vijana wa Kamusinga na Namwela kwa kufuzu kuwakilisha taifa letu katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye mchezo wa magongo na voliboli pasi na kusahau wasichana wa Moi girls Kamusinga ambao watatuwakilisha kwenye handiboli, binafsi nawapongeza walezi wa vipaji kutokea Bungoma,” Bw. Ngugi alisema.

Kikosi cha wavulana cha shule ya upili ya Namwela kimesajili matokeo mazuri katika kipute hicho huku kikifuzu katika semi fainali baada ya kuwatingiza wenzao wa Kamba boys takribani mabao 3-1.

Kikosi hicho hatimaye kiling’aa kwenye nusu fainali dhidi ya kile cha shule ya upili ya St. Joseph kutokea jimbo la Trans Nzoia kwa kuwabamiza na kuwabebesha gunia la mabao matatu komboa ufe.

Kikosi hicho sasa kitawavaa Cheptil hapo Jumatatu 12 Septemba kubaini mbivu na mbichi kwenye nafasi ya kwanza na ya pili huku vikosi hivyo vyote vikiwa vimefuzu kwenye awamu ya Afrika Mashariki.

Viongozi mbalimbali kutokea jimbo la Bungoma wakiongozwa na mbunge wa eneo bunge la Sirisia John Waluke, mwenzake wa Webuye Magharibi Dan Wanyama, yule wa Luanda Dick Maundu na mwenyekiti wa michezo kanda ya Magharibi pamoja na mwenzake wa jimbo la Vihiga wamejiunga pamoja kuvipongeza vikosi hivyo wakielezea imani yao kwamba vikosi hivyo vitajisatiti kupeperusha bendera ya taifa kule Afrika Mashariki.

“Tuna imani kuwa vikosi hivi vitabeba jina la Bungoma vilivyo kwenye kanda ya Afrika Mashariki,” mbunge Waluke alisema.

“Nataka nimpongeze gavana wa jimbo la Bungoma Ken Lusaka na seneta wa sasa Moses Wetang’ula kwa kutoa mchango mkubwa kuhakikisha kuwa vikosi hivi vinapata nafasi katika nashindano haya,” mbunge wa Webuye Magharibi alisema.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa shirikisho la michezo ya shule za upili Bw. Ngugi, kipute hicho cha mashindano ya jumuiya ya Afrika Mashariki kimeratibiwa kutesa nyasi baina ya tarehe 14 na 24 Septemba.

Mwangi Oliver na Roseland Lumwamu 

 

 

Leave a Reply