Wednesday, September 18, 2024
Home > Counties > Bungoma > Ingwe kuwavaa Nzoia ugani Sudi Jumapili hii

Ingwe kuwavaa Nzoia ugani Sudi Jumapili hii

Magwiji wa soka kanda ya magharibi watatifua kivumbi Jumapili hii ugani Sudi Bungoma kuanzia mida ya tisa alasiri.

            Mtanange huo utawakutanisha wasaga sukari wa Nzoia dhidi ya AFC Leopard ukipenda chui ama ingwe kwa jina utani.

Mechi hio ya raundi ya thelathini na tatu itawakutanisha wanangarambe hawa ambao wanapania kuboresha matokeo yao msimu unapokaribia kilele.

 Hadi kufikia sasa Chui wanashikilia nafasi ya sita kwenye jedwali wakiwa wamesakata mechi thelathini na moja na kujizolea  alama arobaini na sita alama kumi na nne nyuma ya Tusker ambao wanashikilia nambari ya kwanza kwenye jedwali.

 Nzoia sugar wanashikilia nafasi ya kumi na tano na alama thelathini na moja alama kumi na tano nyuma ya Chui na ushindi  wa Jumapili utawawezesha kupunguza pengo hilo.

Kwa mujibu ya mitanange mitano ya hapo awali iliyowakutanisha nguli hawa wa soka, Chui wamewabamiza Nzoia Sugar mara moja kwa ushindi finyu wa bao moja komboa ufe.

Nzoia kwa upande wao wameandikisha sare nne dhidi ya Chui ya hivi punde ikiwa sare tasa mnamo tarehe 21/05/2022.

Hata hivyo mkufunzi wa Nzoia Sugar Salim Babu ameelezea matumaini ya wanazoia na kuwahakikishia mashabiki wa Nzoia kuwa vijana wake wamejiandaa vilivyo kabeba ushindi huo muhimu ambao utawahakikishi matumaini ya kusalia kwenye ligi kuu nchini.

Babu ambaye alikabidhiwa mikoba ya nzoia miezi minne iliyopita baada ya kutimukiwa kwa Ibrahim Shikanda ameisaidia Nzoia kuzoa alama sita kwa mechi tano za hivi punde huku wakishinda mechi moja kupiga sare tatu na kutitimwa bao moja kappa dhidi ya Wazito mnamo 15/05/2022.

 Kwa mujibu wa matokeo haya, Babu hajapoteza katika mitanange nne ya hivi punde na anapania kuendeleza msururu huo wa matokeo bora.

Ingwe kwa upande wao wameandikisha matokeo bora katika mechi tano za awali wakiwa wamevuna ushindi mara mbili dhidi ya Kakamemega Homeboyz na FC Talanta mtawalia na kuvuna sare dhidi ya City Stars, Nzoia na Gor Mahia. Bila shaka ingwe watapania kulinda rekodi yao ya kutopoteza  na kupambana kufa mtu almuradi wapande kwenye jedwali.

Nahodha wa Nzoia Humphrey Katasi alizungumza na KNA kwa njia ya simu na kuwaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi haswa ikizingatiwa kuwa mechi hio itaandaliwa katika uga wa nyumbani.

 Katasi pia aliwataja Ingwe kama timu nzuri ambayo inapania kuendeleza rekodi lakini akasema kamwe Nzoia hawatishwi na kucha za Chui ikizingatiwa kuwa Chui hawajaandikisha ushindi dhidi yao  katika mechi tano za awali.  

Kwa upande waje mkufunzi wa Ingwe Patrick Aussems ambaye amehudumu tangia alipofungishwa virago Anthony Kimani Modo , ushindi wa Ingwe ni lazima kama ibada kwa kuwa Ingwe ni tiumu Kubwa na ni sharti idhihirishe ukubwa wao wa soka.

Na Oliver Mwangi and Roseland Lumwamu 

 

Leave a Reply