Kituo cha kuwarekebisha wakazi waliolemewa na pombe na dawa za kulevya kilichojengwa na shirika la NACADA kwa gharama ya Sh9 milioni katika kaunti ya Elgeyo Marakwet kitaanza kuwahudumia wakazi Januari mwaka 2020.
Mwanakamati kuu ya kaunti anayesimamia afya, Kiprono Chepkok alisema kaunti hiyo ina watalaam wa kutosha kutoa huduma kwa wakazi katika kituo hicho ambacho kinaweza kuwahudumia watu 30 kwa wakati mmoja.
Mwanakamati huyo alisema kaunti kwa sasa ina watalaam wawili wa tiba ya akili na wauguzi kadhaa waliosomea saikolojia na magonjwa mengine ya kiakili.
Kiprono aliyekuwa akiongea wakati alipokea kituo hicho kutoka kwa idara ya wafanyikazi wa umma alisema kituo hicho kina nafasi ya wanawake 15 na wanaume 15.
Alisema kituo hicho kitakuwa wazi kwa wakazi wote walio na tatizo la unywaji pombe kupindukia na utumizi wa dawa za kulevya lakini akasema kufikia sasa, idara yake haijakadiria fedha zitakazotozwa.
Alisema kaunti imeandaa mazungumzo na bima ya afya nchini NHIF kuona kama wanaweza pia kufadhili wagonjwa akisema huu ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine wowote ule.
Hata hivyo, alisema kituo hicho bado kinahitaji fedha zaidi akisema bado hakina vifaa vya kuwahudumia wateja wake lakini akaeleza matumaini yake kwamba watakuwa wamevipata watakapoanza kutoa huduma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Emedau Papa ambaye ni mmoja wa watalaam wa akili alisema kaunti hiyo imeendelea kuwapoteza wafanyi kazi wengi kwa unywaji pombe na utumiaji wa dawa za kulevya ilihali wanaweza kusaidiwa.
Alisema hili linamaanisha kupoteza rasilmali muhimu kwa kaunti, na pia kaunti kupoteza mapato kutokana na wakati mwingi watu walio na tatizo hilo wanatumia bila kutoa huduma yoyote wanapokuwa wamelewa.
Mkurugenzi wa idara inayosimamia pombe Joshua Cherop alisema wameona jinsi vituo kama hivyo vimesaidia wakazi wengi waliorudia maisha yao ya kawaida na kusema wana matumaini kwamba wengi watanufaika kwani huduma hizo kwa sasa zitakuwa karibu.
Hivi majuzi, maafisa wanaosimamia urekebishaji tabia waliitaka kaunti kuanza kutoa huduma katika kituo hicho wakisema wengi wanaopewa kifungo cha nje ni wale wanaoshiriki unywaji pombe na utumiaji wa dawa za kulevya.
Na Alice Wanjiru