Saturday, October 12, 2024
Home > Counties > Bungoma > Spika wa Bunge atunukiwa shahada ya udaktari

Spika wa Bunge atunukiwa shahada ya udaktari

Spika wa Bunge, Moses Wetang’ula mnamo Ijumaa alitunukiwa shahada maalum ya uzamifu almarufu Doctor of Human Letters na Chuo Kikuu cha Kibabii wakati wa mahafala ya saba ya kuhitimu katika taasisi hiyo.

Hapo awali alijulikana kama Mhe. Moses Francis Masika Wetang’ula, bali sasa salamu zake zinabadilika na kujumuisha shahada yake, Mhe. (Dkt.) Moses Francis Masika Wetang’ula.

Katika hotuba yake ya kuitikia shahada hiyo, Spika Wetang’ula alisema alihisi kunyenyekea kwa ishara hiyo na alishukuru usimamizi wa Chuo Kikuu cha Kibabii kwa heshima hiyo ya kipekee.

“Heshima hii sio tu onyesho la mafanikio yangu binafsi, lakini pia ni uthibitisho wa bidii na juhudi za watu wengi ambao wameniunga mkono na kunitia moyo katika safari yangu hadi sasa,” alisema.

Spika aliahidi kuendelea kujipa changamoto kwa nia ya kufikia viwango vipya vya ubora, na kuwatia moyo wengine kufanya hivyo.

Alimshukuru Mungu akisema kwamba yeye daima hupata motisha kutokana na maombi katika shughuli zake.

“Ninapopata heshima hii leo natafuta faraja kwa maneno ya Reinhold Niebuhr, ambaye ninajikita katika maombi yake kwamba,”Mungu nipe utulivu wa kukubali mambo ambayo siwezi kubadilisha, ujasiri wa kubadilisha mambo ninayoweza na hekima ya kujua tofauti,” alisema Bw Wetang’ula.

Daktari Wetang’ula hata hivyo aliungana na viongozi wengine mbalimbali nchini kulaani uamuzi wa mahakama ya upeo kuhusu ombi la jamii ya LGBTQ kusajiliwa kama muungano na bodi ya mashirika yasiyo ya kiserilikali.

Alitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume cha maadili na kusistiza kuwa haikubaliki kwa watu wa jinsia moja kujamiana.

“Nataka kuungana na Wakenya wote, Wabunge na uongozi wa nchi unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt William Ruto kuwaambia wapotovu hao wa LGBTQ kwamba kama wanataka kujenga Sodoma na Gomora ya kisasa nchini Kenya, Serikali ya Kenya Kwanza itaipinga kwa nguvu zote,” alisema.

Spika wa Bunge la Kitaifa pia alibainisha kuwa wapotovu wa kijamii na wale ambao hawawezi kuangamiza viumbe wa kiume na wa kike maishani hawana nafasi katika jamii.

Na Roseland Lumwamu

Leave a Reply