Wednesday, December 11, 2024
Home > Education > Tolgos amwomboleza Moi

Tolgos amwomboleza Moi

Gavana  wa Elgeyo Marakwet, Alex  Tolgos  ametuma rambirambi zake kwa familia, jamaa, marafiki na wakenya wote kwa jumla kufuatia kifo cha rais mstaafu, Daniel Toroitich arap Moi.

Tolgos alisema rais mstaafu alikuwa na uhusiano wa kipekee na kaunti hiyo ikizingatiwa kwamba aliingia katika uongozi wa kitaifa kutoka chuo cha Tambach ambako alikuwa mwalimu.

“Itakumbukwa kwamba, Mzee Moi alikuwa mwalimu katika chuo cha Tambach hapa Elgeyo Marakwet kabla ya kuteuliwa kujiunga na baraza la Legco (Legistlative Council of Kenya) na kutokea hapo kujiunga na uongozi wa kitaifa,” alisema Tolgos.

Tolgos aliendelea kusema kuwa wakazi wa kaunti hiyo walikuwa na uhusiano wa karibu na rais mstaafu akisema nyumba alimoishi kule Tambach bado ipo na imekuwa kumbukumbu inayoasihira neema ya mwenyezi Mungu kwa mwalimu mnyenyekevu aliyeinuliwa na kuiongoza nchi kwa muda wa miaka 24.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, gavana huyo alisema katika ziara yake ya mwisho kwa kaunti hiyo Moi aliwashauri viongozi kuyajali maisha ya vizazi vijavyo kwa kuwekeza kwa elimu.

Wengine waliotoa rambirambi zao ni pamoja na mwakilishi wodi ya Embobut/Embolot, Paul Kipyatich aliyetaka viongozi waige mfano wa Moi wa kutafuta umoja wa kitaifa.

Na  Alice  Wanjiru

Leave a Reply