Friday, September 13, 2024
Home > Education > Wadau wa Kiswahili wakongamana Mombasa

Wadau wa Kiswahili wakongamana Mombasa

Wadau wa lughaya Kiswahili barani Africa walikongamana jijini Mombasa Ijumaa kutaathmini kikulacho Kiswahili kwa karne nyingi tangu kizinduliwe Afrika Mashariki.
Kongamano hilo la dunia kwa nembo “Koja la walumbi wa Kiswahili duniani” lilinuia kuwarai wasomi kutambua lugha ya Kiswahili kama lugha tambulika kwenye Nyanja za wasomi watajika.
Kongamano hilo liliwahamasisha Wafrika na dunia nzima kujua umuhimu wa lugha ya kujivunia ya Afrika pasipokutegemea lugha za ugenini.

Mgeni rasmi wa koja hilo Athman Hussein aliye Mkurugenzi Msaidizi hitifaki za kitaifa Kenya aliwarai wanagenzi kutilia maanani lugha, somo na tamaduni za Kiswahili kwani kuna nafasi ya Kiswahili kutambuliwa kuwa lugha rasmi ya bara la Afrika kwenye malengo ya riwaza la Africa 2063.

Miswada katika jumuia ya Afrika na umoja wa kimataifa zina lengo la kuhalalisha mojawapo katika lugha ya Kiswahili na Kiarabu kutumika kama lugha rasmi ya Afrika.
Mwandishi mtajika Wala Bin Wala wa kituo cha Kiswahili Kenya alizomea wale watu wasiojivunia lugha ya Kiswahili kwa kuzienzi lugha za wengine.

“Mimi najivunia lugha ya Kiswahili kwani ninunuapo gazeti siku yoyote ile mimi huagiza kwanza gazeti la Taifa Leo kabla ya mengine,” bin Wala alinukuliwa kwenye usemi wake kwenye koja hilo.

Hili jambo limechangia sana kudorora kwa Kiswahili humu nchini Kenya na maeneo mengine kusudi kwamba mmoja akiongea Kiswahili barazani au kwenye vyombo vya habari ataonekana kama asiyekuwa na masomo.

Wazazi pia walihimizwa wawaelekeze watoto wao kwenye Nyanja ya uswahili kwani Kiswahili kina nafasi nyingi za ajira zikiwemo Ukalimani, uandishi, utangazaji, kuigiza, nyimbo, filamu na zinginezo.

Afrika kusini ipo kwenye mikakati ya kuanzisha somo la Kiswahili kwenye vyuo na shule baada ya kugundua uwezo wa lugha hii.

Bin Wala alisema watu wengi wakiwemo wasomi, watangazaji, waalimu, wanasiasa wanachangia kutotambulika kwa lugha ya Kiswahili kwa kuzienzi lugha za kigeni.

Kutojumulishwa kwa Kabila la Waswahili kama mojawapo wa makabila ya Kenya 42 ni jambo lililohusishwa na kudidimia kwa lugha yenyewe.

Wadau waliliuliza swali bila kupata jibu la, je, kutakuwaje na kofu bila embe? Kumaanisha kwamba lugha ya Kiswahili inafaa kuwa na wenyeji wake.

Ilibainika wazi kwamba kanuni, mila na tamaduni za waswahili zimetambulika na kwa hivyo kabila la Waswahili litakipa kipau mbele swala la kuhalalisha Kiswahili na miundo msingi yakukiendeleza kwa siku zijazo.

Uchunguzi wa kina ulipendekezwa ili kubainisha mwanzo wa Kiswahili haswa ni wapi kadri ya zile potovu zilizo andikwa na watu tatanishi kutoka nchi za nje.

Wadau walikubaliana kwamba kuna uhusiano mkubwa wa Kiswahili na pwani ya Afrika mashariki toka kusini mwa Somalia hadi kaskazini mwa Msumbiji wakiagiza uchungizi wa kina kutatua na kurekodi wapi haswa Kiswahili kilianzia.

Kwenye kongamano hilo kitabu kipya cha Kiswahili Fasihi ya Ufungwa, kilicho andikwa na Zuhura Said na Abdulrahim Hussein Taib kilizinduliwa na Mgeni rasmi Bw. Athman Hussein hapo jana.
Nchi zilizowakilishwa kwa wingi Zikiwemo wenyeji Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Congo, Zanzibari, Ghana na zinginezo.

Na Joseph Kamolo

Leave a Reply