Sunday, May 19, 2024
Home > Counties > Wahudumu wa matatu wahofia kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya korona

Wahudumu wa matatu wahofia kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya korona

Wahudumu wa matatu eneo la Molo sasa wanaitaka serikali kuwapa mahala mbadala pa kuendeshea biashara yao kwani pale walipewa pana hatarisha maisha yao kutokana na kuzuka kwa maradhi ya covid-19.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Railways ambapo imewekwa kama steji ya muda, dereva mmoja wa matatu Isaac Ngige alisema kuwa mahala hapo ni pa dogo mno kiasi cha kwamba wanashindwa kuweka mikakati kabambe ya kuzuia maambukizi ya covid-19 hasa ile ya kuweka umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Ngige aliendelea kusema kuwa hali hii inawatia wasiwasi ikizingatiwa kuwa wanasafirisha mamia ya watu kila siku na hivyo basi kuomba kupatikana kwa suluhu mwafaka kwa haraka. Kwa upande wake, anaonelea ingekuwa vyema iwapo kila shirika la matatu lingeleta gari moja moja mahala pale ili kuzuia msongamano.
Hata hivyo, Ngige alisema kuwa wamejaribu vilivyo kuhakikisha kuwa wazo hili linatekelezwa lakini alilalamikia kunyanyaswa na maafisa wa polisi ambao hawawakubali kuweka matatu zao mahala pengine isipokuwa hapo Railways.
Awali, matatu hizi zilikuwa zimetolewa katika steji zao za kawaida na kuhamishwa hadi uwanja wa Molo ambako walilalamikia mazingara mabovu ya kazi, kutokuwa na maji, na pahali pa kujisaidia, barabara mbovu iliyofanya magari kukwama, uwanja kulowa maji na hivyo basi kuhamishwa tena hadi Railways.
Kwa mujibu wa mhudumu Benson Towett, hali hii inaendelea kuwahofisha zaidi lakini iwapo swala la msongamano huu litasuluhishwa basi watakuwa hata na wepesi kwa kuifanya kazi yao bila manung’uniko yoyote.
Towett alisema kuwa wamejaribu kadri wawezavyo kufuata masharti yanayotolewa na serikali kama vile kuweka maji ya kunawa, kubeba abiria wanaohitajika kwa matatu lakini ile ya kukaa umbali wa mita moja na mwingine imekuwa ngumu na hivyo basi kuiomba serikali kuliangalia swala hili kwa kina ili kuyaokoa maisha ya wengi kwa kutoambukizwa virusi vya covid-19.
Kisa cha kwanza cha mgonjwa kupatikana na virusi vya covid-19 nchini Kenya kilitangazwa mnamo mwezi Machi 13, mwaka huu na tangu wakati huo, serikali imeendelea kuweka mikakati kuhakikisha kuwa virusi hivi havienei kwa upesi.
Baadhi ya wale wanaohitajika kuhakikisha kuwa wanafuata masharti haya kikamilifu ni wanaohudumu katika sekta ya usafiri ikiwemo wa wahudumu wa matatu na waendeshaji boda boda. Kwa wengi, hatua hizi zimewaathiri kiuchumi lakini hawana budi ila kutekeleza yale yanayohitajika.

Na Emily Kadzo

Leave a Reply