Waakazi wa Mombasa wameeleza kushtuka kwao na kifo cha Rais mstaafu Daniel arap Moi kilichotokea siku ya Jumanne asubuhi katika hospitali ya Nairobi.
Wengi wa wale waliozungumza na shirika la habari la Kenya, KNA walimtaja Mzee Moi kama kiongozi aliyetumikia Kenya kwa moyo wake wote.
“Raisi Moi alitumikia nchi yetu kwa dhati na kuwapenda wakenya wote bila kujali misingi yao ya kikabila, dini au rangi, Alisema Mwalimu mstaafu wa chuo cha mafunzo ya walimu cha Shanzu, Mariam Issa.
Bi Issa alisema Mzee Moi atakumbukwa kwa kujitolea kwake kuimarisha hali ya elimu humu nchini na kuhakikisha kila mtoto amepata haki sawa ya kielimu.
Aliyekuwa Meya wa Mombasa, Rajab Sumba alimtaja Mzee Moi kama kiongozi mzalendo aliyeunganisha makabila yote ya Kenya.
“Wakati nilipokuwa meya, nilifanya kazi kwa karibu sana na Moi wakati huo akiwa Raisi wa Kenya na alipenda sana watu wa pwani,” alisema Sumba.
Meya huyo wa zamani alisema ni wakati wa uongozi wa Raisi Moi, wapwani walipata nyadhifa muhimu katika serikali na taasisi zingine za umma.
“Mfano mzuri ni kuchaguliwa kwa Phares Kuindwa kama mkuu wa utumishi wa umma na katibu katika baraza la mawaziri, aliongeza kusema meya huyo wa zamani.
Pia alisema Moi alifanya ziara za mara kwa mara katika mji wa Mombasa na pwani kwa jumla na kuanzisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Aliyekuwa naibu wa waziri wa elimu na mbunge wa Malindi, Abubakar Badawy alimtaja Raisi Moi kama kiongozi aliyekuwa na huruma kwa watu wake na pia mzalendo wa hali ya juu.
“Mwito wake wa amani, umoja na upendo uliwezesha kuwaunganisha wakenya. Moi atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri aliyofanyia nchi hii,Alisema Badawy.
Alisema Moi alijitolea mhanga kuona wakenya hasa wale maskini wanaimarika kimaisha kwa kuanzisha miradi mbali mbali ya Nyayo.
Alitaja kifo chake kama pigo kubwa kwa Kenya na bara zima la Afrika.
By Mohamed Hassan