Wednesday, December 4, 2024
Home > Counties > Wakaazi wa Pokot Magharibi washabikia Dawa za kiasili

Wakaazi wa Pokot Magharibi washabikia Dawa za kiasili

Dawa za kiasili zina umaarufu wake katika sekta ya matibabu ulimwenguni huku mabadiliko ya kiteknolojia na utamaduni yakiwafanya watu wengi kuangazia dawa za kisasa.

Hata hivyo kutokana na ongezeko ya maradhi sugu kama vile saratani nchini, baadhi ya waathiriwa wameona afueni katika kurejelea tiba za kiasili ambazo zimetajwa kuwa za bei nafuu na salama.

Katika kaunti ya Pokot Magharibi, dawa hizo za kiasili bado zina mashiko huku wakaazi wakizishabikia kama tiba kwa maradhi ya aina mbalimbali hata ingawa kuna wale wanaoziona kama zilizopitwa na wakati.

Hii inadhihirika wazi unapozuru masoko ambapo kuna hata sehemu maalum dawa hizo huuzwa kwa wateja, hali ambayo ni nadra kuishuhudia katika sehemu nyingine za nchi hasa mijini.

Hali kadhalika mna wataalamu si haba wanaotoa huduma hizo za dawa za kiasili ambao wamefungua vioski maalumu kwa shughuli ya kuuza dawa hizo inavyodhihirika katika mji wa Kapenguria pamoja na miji mingine katika kaunti.

Pia unaposaili wenyeji wa kaunti hii kule kunakopatikana dawa hizo za kienyeji hawatakosa kukufahamisha wataalamu ambao wameendesha shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya kaunti.

Wenyeji hao wanaamini kuwa kuna wale watu maarufu kuliko wengine katika sekta hiyo ya tiba za kiasili na huwa hawajigambi wanapoendesha shughuli zao tofauti na wengine ambao wanakisiwa kuwa na tamaa ya pesa.

Samson Kisur, ambaye anadai kutumia dawa za kiasili kwa miaka mingi pamoja na familia yake, anasema kuwa hajaona dosari yoyote kwa dawa hizo.

“Nilikuwa na kijana yangu ambaye alikuwa anasumbuliwa na homa kali pamoja na kuumwa na kifua kila mara akiwa mtoto. Nilishauriwa kutafuta dawa za kiasili kutoka kwa mtaalamu mmoja katika sehemu hii na hadi wakati huo kijana yangu yuko imara kiafya,” alisema Kisur.

Alisisitiza kuwa tangu wakati huo yeye hutumia dawa za kiasili na hospitalini yeye huenda tu huko kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na baadaye kutafuta dawa kutoka kwa wahudumu wa dawa za kiasili.

“Wakati mwingi si lazima kufanyiwa uchunguzi maana hao wahudumu wa dawa za kiasili wana uwezo wa kudadisi na kuutambua ugonjwa wanaugua wateja wao,” alieleza, hisia zinazoandamana na watumizi wengine wa dawa hizo.

Alidai kuwa watu wengi wanaogopa kutumia dawa za kiasili kutokana na ongezeko la wataalamu bandia ambao hawana ujuzi wala vipawa vya kuwa matabibu wa kiasili.

Richard Loitang’ole, ambaye ni mhudumu mmoja wa dawa za kiasili anasema aliamua kufungua zahanati nyumbani kwake katika kata ya Lityei, baada ya mchipuko wa janga la korona.

Richard Lotang’ole akiwa katika kliniki yake. Picha Na Richard Muhambe

Lotang’ole anasema amekuwa mhudumu wa dawa za kiasili kwa zaidi ya miaka 30 lakini alianzisha zahanati kwa jina Ketnyo katika mji wa Chepareria mnamo mwaka wa 2015 na baadaye mji wa Makutano kabla ya kuihamisha tena mwaka jana.

Anaeleza kuwa amekuwa akiwahudumia wagonjwa wengi kwa kipindi hicho chote wakiwemo wanaougua saratani ambapo wamerejelea afya yao nzuri.

“Nilirithi utaalamu huu kutoka kwa nyanya wangu wawili yaani wa upande wa mama na ule wa baba. Yule wa upande wa baba alikuwa anatibu homa ya matumbo na malaria huku nyanya wa upande wa mama akiwa anashughulikia ugonjwa wa saratani na vidonda sugu,” alifafanua Lotang’ole.

Alisema alijitosa katika ulingo wa dawa za kiasili akiwa mtoto mdogo ambapo mara kwa mara nyanya wake walikuwa wanamtuma msituni kutafuta mizizi na matawi ya kutengeneza dawa.

Mhudumu huyo ameajiri madaktari wenye ujuzi katika upasuaji na anashirikiana na vituo vya afya katika shughuli za kuwashughulikia magonjwa mbalimbali.

“Inawachukua wagonjwa wa saratani ujasiri na imani kutukia dawa za kienyeji kutokana na fikira kwamba mgonjwa wa saratani hawezi pona,” alisema.

Christine Chebore ni mtaalamu mwingine wa dawa za kiasili ambaye anaendesha huduma zake katika soko la Makutano mjini Kapenguria ambapo amejikita katika utoaji wa dawa za kutibu homa ya matumbo, ugonjwa wa maziwa (brucella), malaria, maumivu ya mgongo, maradhi ya figo pamoja na mengine, ujuzi anaosema aliurithi kutoka kwa nyanyake.

Alidai kuwa dawa zake zilimfanya jamaa yake aliyepatikana na virusi vya korona kurejelea hali yake nzuri ya kiafya baada ya muda mchache.

Anakadiria kuwa kuna wahudumu wa dawa za kiasili wengi ambao serikali inapaswa kuwajumuisha katika sekta ya matibabu kwa sababu wanachangia pakubwa katika kutoa tiba kwa magonjwa sugu hata ya kisasa.

“Tungependa serikali ya kaunti pamoja na ile ya kitaifa kututambua kwa kufadhili utafiti pamoja na kutoa vibanda bila kutozwa ushuru kwa minajilli ya shughuli zao,” alisihi Bi Chebore.

Wataalamu hao wanashikilia msimamo kuwa dawa za kiasili hazina madhara kiafya ikilinganishwa na zile za kisasa ambazo huwa na kemikali zenye kuathiri watumizi baada ya kuzitumia kwa muda mrefu.

Changamoto kubwa inaowakabili wataaalamu hao wa dawa za kiasili wanasema ni ongezeko la uharibifu wa misitu pamoja na kilimo kwa ujumla ambapo baadhi ya miti na mimea iliyo nadra sana kupatikana inaendelea kupotea.

Walisema kuna haja ya serikali kuangazia maeneo ambayo yanaota miti na mimea fulani ili yasije kubadilisha hali yao ya asili pamoja na kuchukulia hatua kali wale wanaokata miti ya kiasili ili kuchoma makaa.

Hali kadhalika wanashikilia kuwa iwapo tiba za kiasili zitaimarishwa, kaunti ya Pokot Magharibi itatambulika katika utalii wa kimatibabu ambapo watu kutoka sehemu nyingine za nchi na hata nchi za ughaibuni watazuru eneo hilo.

Na Richard Muhambe

Leave a Reply