Tuesday, October 8, 2024
Home > Counties > Wakulima wahimizwa kupanda mimea mbadala

Wakulima wahimizwa kupanda mimea mbadala

Wakulima katika kaunti ndogo ya Bungoma Kusini wamehimizwa kupanda mimea mbadala na kushughulika na kilimo biashara ambacho kitaboresha maisha yao.

Akizungumza katika mahojiano na KNA katika afisi yake hapo jana, afisa wa Kilimo wa Kaunti ndogo ya Bungoma kusini David Shivonje amewarai wakuluma kupanda mimea mingine kama vile wimbi, mtama, njugu, ndengu, mihogo, mboga za kienyeji na mingineyo kando na mahindi.

Shivonje aliwashauri wakulima kuwa baadhi ya mimea hii inachukua muda mchache kukomaa na kuwa tayari kuuzwa sokoni ili kuwaletea wakulima manufaa katika maisha yao.

Aliwataka wakulima kujiunga katika vikundi ili waweze kuyasafirisha mazao yao katika miji mikuu kama vile Nairobi na Mombasa ambapo yatauzwa kwa bei nzuri na kuboresha maisha ya wakulima.

Aidha alisema kuwa kwa kutumia vikundi, wakulima hawo watapunguza gharama za usafirishaji wa mazao yao kuliko mkulima akifanya hivyo kibinafsi.

Aliwahimiza afisa wengine wa kilimo wa nyanjani kuhakikisha kuwa wanawaelimisha wakulima kulingana na kanuni na masharti ambayo wanafaa kuzingatia kwa kukuza mimea hiyo ili wapate mazao mwafaka ambayo wanaweza kuuza na masalio yauzwe sokoni kupitia kwa vikundi.

Afisa huyo wa kilimo amewataka wakulima wote kuzingatia masharti yote ya kilimo kama vile kuandaa shamba kwa wakati unaofaa, kupima mchanga wao ili wajue mbolea inayofaa kutumiwa kwa mashamba yao, na kupalilia mimea kwa wakati unaofaa iliwapate mazao bora na mengi.

Alisema kuwa kando na kukula ugali wa mahindi wakaazi wakitumia ugali wa wimbi au mtama na vyakula vingine afya yao itaimarika na watakuwa na nguvu na magonjwa hayataonekana karibu nao.

Na Maureen Imbayi

 

Leave a Reply