Friday, November 8, 2024
Home > Counties > Wanariadha wapokea usaidizi

Wanariadha wapokea usaidizi

Wanariadha wanaoendelea kukita kambi mjini Iten walinufaika na msaada wa vyakula kutoka kwa wahisani mbali mbali.
Mfanyibiashara Kiprono Barmasai alisema alianzisha shughuli hiyo baada ya kuona jinsi wengi wa wanariadha ambao ni wateja wake wanavyoteseka baada ya kukosa njia za kujipatia riziki kufuatia kusitishwa kwa mashindano ya mbio mbali mbali kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.
Alisema alipata chakula kutoka kwa mhisani mmoja lakini alipojaribu kugawa alishtuka alipopata mamia walihitaji msaada na ikambidi kutafuta wahisani wengine.
Juhudi zake zilizaa matunda baada ya serikali ya kaunti, makocha na wafanyi biashara kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet walipoungana na kutoa mchango wao.
Kocha Elkanah Ruto alisema wanariadha 700 walijisajili kutafuta msaada na ilibidi kuwachuja ili kubaki na wanariadha 170 kulingana na msaada waliokuwa nao.
“Tuliwapa kipao mbele wanariadha walio na familia zinazowategemea, wale wa kigeni waliofungiwa hapa na janga hili la Corona na wakazi ambao si wanariadha lakini wanaishi na ulemavu,” alisema Kocha Ruto.
Mmoja wa wanariadha wa kigeni waliofaidika ni Brian Hannington kutoka nchi jirani ya Uganda ambaye alielezea furaha yake kupata usaidizi huo.
“Sikutarajia kupata chakula, hili ni jambo la kushangaza kwangu na nawashukuru wahisani wote kwa kutufikiria sisi kwani janga hili halibagui uraia wa mtu bali wote tumeathiriwa,” alisema Hannington.
Hannington alisema amekuwa akikabiliwa na changamoto tele zikiwemo ulipaji wa kodi na kununua chakula baada ya kufungiwa kurudi kwao na janga hili la corona.
“Nilikamilisha shule mwaka jana na nikaja Kenya nikitarajia nitafanya mazoezi yatakayoniwezesha kushiriki kwa mbio mbali mbali ili niweze kupata riziki jambo ambalo halikuwezekana sasa,” alisimulia mwanariadha huyo.
Mwanariadha wa zamani Erastus Limo alisema wanariadha wengi wanaendelea kuteseka kwani hawana kazi mbadala isipokuwa riadha.
Mwanakamati kuu anayesimamia michezo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet Anita Kimwatan aliwaomba wahisani kuendelea kujitokeza kuwasaidia wanariadha akisema idadi kubwa bado wanahitaji msaada.
Na Alice Wanjiru

Leave a Reply