Wenyeji wa Mandera wahimizwa kuchukua kadi zao za Huduma

Counties Editor's Pick Governance Mandera

Wakaaji wa kaunti ya Mandera wamehimizwa kuchukua kadi zao za huduma namba.

Kamishna wa kaunti ya Mandera Onesmus Kyatha alisema kwamba wenyeji wengi hawajachukua kadi zao hata baada ya kupata ujumbe wa kuwaelekeza jinsi ya kupata kadi hizo.

Kyatha alielezea kwamba kati ya kadi 22,377 zilizofika 12,906 pekee ndizo zimechukuliwa na wenyewe kufikia sasa.

Alisema kuwa kadi hizi zitatumika kama vitambulisho rasmi kwa raia wote nchini pamoja na wale wa kigeni wanaoishi humu nchini katika kutafuta huduma kwenye afisi za umma.

Kyatha aliwahimiza wale ambao hawakusajiliwa katika awamu ya kwanza kujitayarisha kwa awamu ya pili ambayo alisema itazinduliwa na serikali hivi karibuni.

Aidha aliwaarifu wenyeji kujibu jumbe fupi zinazotumwa kwa simu zao kuhusu eneo karibu la kupokea kadi zao.

Hata hivyo alisema kuwa serikali kupitia machifu inahakikisha kuwa kila mwananchi anafahamishwa kuhusu umuhimu wa kadi hii.

Rais Uhuru Kenyatta na Mama Taifa Margaret Kenyatta walikuwa wa kwanza kupata kadi hizo mnamo Oktoba 20 mwaka jana, wakati wa sherehe za Mashujaa katika uwanja wa Gusii mjini Kisii.

Kadi za Huduma zinatarajiwa kutumika kama vitambulisho rasmi kuanzia mwaka ujao.

Na Charles Matacho

Leave a Reply