Friday, September 29, 2023
Home > Counties > Bunduki haramu 30 zatwaliwa na serikali

Bunduki haramu 30 zatwaliwa na serikali

Serikali imefanikiwa kutwaa zaidi ya bunduki haramu thelathini zilizokuwa zinamilikiwa na raia katika sehemu ya Marsabit ya Kati, jimboni Marsabit.

Naibu Kamishna wa sehemu hiyo, Patrick Muriira alisema kuwa silaha hizo zilitwaliwa na vyombo vya dola kwa sababu zilikuwa zinamilikiwa kinyume cha sheria.

Muriira aliongezea kusema kuwa msako wa kupokonya raia silaha haramu unaoendeshwa na vyombo vya usalama kote jimboni umefanikiwa pakubwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Akiongea na waaandishi wa habari, ijumaa, mjini Marsabit naibu kamishna huyo amehoji kwamba kutokana na mikakati ambayo imewekwa na vyombo vya usalama pamoja na ushirikiano katoka kwa raia,hali ya usalama katika sehemu ya Marsabit ya kati imeimarika.

Oparesheni hiyo ilianzishwa na serikali baada ya visa vya utovu wa usalama kushuhudiwa katika sehemu za Kokuto na Jaldesa.

Aliongezea kusema kuwa misururu ya mikutano ya kujenga amani, kuleta utangamano na maridhiano kati ya jamii mbali mbali zinazoishi katika kaunti hii ndogo inashugulikiwa.

Muriira alisema kuwa vikosi vya polisi vinashika doria ili kuhakikisha ya kwamba hali kamili inadumishwa.

Wakati huo huo alipuuzilia mbali dhana kwamba hatua ya serikali kupokonya polisi wa akiba bunduki walizokuwa wamekabidhiwa na serikali huenda imechangia kudorora kwa usalama.

Visa vya wizi wa mifugo vimekuwa vikishuhudiwa mara kwa mara katika eneo hilo lakini serikali imeweza kudhibiti hali hiyo.

Naibu huyo wa kamishna hata hivyo alidokeza kuwa serikali inaendelea kutathimini swala hilo ilikuhakiki iwapo polisi hao wa ziada watarejeshewa silaha au la.

 

Na Sebastian Miriti

 

 

 

Leave a Reply