Friday, September 20, 2024
Home > Counties > Bungoma > Bungoma yamezea mate uzinduzi wa miradi Kisumu

Bungoma yamezea mate uzinduzi wa miradi Kisumu

Baada ya miaka mingi ya kusahaulika, Kisumu na Luo Nyanza sasa wanavuna makubwa kutoka kwa utawala wa Jubilee wa Rais Uhuru Kenyatta katika uzinduzi wa miradi mbalimbali.

Hali hii imeifanya kaunti ya Bungoma kutamani pia nao kuandaa siku kuu siku za usoni.

Hapo awali serikali ilifanya mikakati ya kuwepo kwa mzunguko wa kuandaa siku kuu katika kila kaunti.

Mwaka huu, siku kuu ya Madaraka ilifanyika katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu.

Rais Kenyata alisafiri kuelekea jiji la Kisumu Jumapili, ambapo alijiunga na mwenyeji, aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, kabla ya sherehe za Madaraka siku ya jana Jumanne.

Mbali na maendeleo ya miundombinu kama barabara ambazo rais alianza kuzindua Jumapili, ziara yake ya jiji ilileta furaha kwa wengi, na ukuaji wa uchumi uliorekodiwa katika tasnia ya hoteli.

Wakaazi wa kaunti ya Bungoma walieleza kuwa watakapomwalika Rais pia katika kaunti yao kutakuwa na maendeleo kabambe kama wanavyonufaika sasa kaunti ya Kisumu.

Wengi walisisitiza kuwa hata ikiwezekana siku kuu inayofuata iandaliwe katika kaunti ya Bungoma.

Jambo hilo kwa kiwango fulani limekuwa gumu kwa kaunti ya Bungoma kuandaa siku kuu,wengi wakisema kuwa bado kuna miradi ambayo haijakamilika kwa sasa ikiwemo uwanja wa michezo wa Kanduyi.

“Siku ya Madaraka haisherehekewi tu kama sherehe, pia inakuja na mambo mengi mazuri ambayo Mheshimiwa Rais anakuja nayo, ” alisema Philip Simiyu, mkaazi wa Bungoma huku akiongeza kuwa ni dhahiri shahiri kuwa mwaliko wa Rais katika kaunti yeyote ile, huleta manufaa ya uzinduzi wa miradi mbalimbali.

“Ili kaunti liweze kuandaa siku kuu kuna mambo mbalimbali ambayo lazima yashughulikiwe. Usalama ni moja ya mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaombele. Suala la ukumbi pia linapaswa kushughulikiwa kwa kuwa ni hafla kubwa inayohudhuriwa na wengi,” Alisema mwanaharakati,Nahashon Mwakazi.

Wenyeji wa Bungoma wamejitokeza pia na kusema nao pia wanatamani kuonja matunda ya “Handshake” kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kama vile kaunti ya Kisumu na maeneo ya mkoani Nyanza wanavyonufaika sasa.

Walisema kwa mfano wangetaka kuona uwanja wa michezo wa Kanduyi ukiwa umekamilika ndipo vijana wenye talanta ya kujihusisha na michezo mbalimbali waweze kuendeleza vipaji vyao.

Na Dishon Amanya

Leave a Reply