Saturday, February 15, 2025
Home > Counties > Mlo wa sumu wasababisha maafa Kuresoi 

Mlo wa sumu wasababisha maafa Kuresoi 

Siku moja tu baada ya serikali ya kaunti ya Nakuru kuwaonya wakazi wa Kuresoi Kusini dhidi ya kula nyama ambayo haijakaguliwa na afisa wa afya kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa kimeta na kichaa cha mbwa, mvulana mmoja wa miaka kumi aliaga dunia kwa kukiuka hilo agizo.

Kwa mujibu wa wakazi  wa kijiji hicho cha Tinet, mwendazake aliibugia supu ya mifupa iliyokuwa imetengenezwa kutoka kwa nyama ya ng’ombe aliyefariki baada ya kuugua homa ya pwani ya mashariki almaarufu’ east coast fever’.

Wakazi wengine zaidi ya 30 walioshiriki mlo huu wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya gatuzi dogo la Olenguruone baada ya kupata dalili za kusokotwa na tumbo, kuendesha na maumivu mwilini.

Naibu gavana, David Kones aliyetembelea waathiriwa katika kituo hicho cha afya, aliwaomba wakazi kutilia maanani maagizo yanayotolewa ili kuepukana na visa kama hivyo mbeleni akisisitiza kuwa agizo lililotolewa jana kupitia wizara ya kilimo ya kaunti bado lingalipo hadi pale magonjwa haya yatakapoisha.

Kones aliendelea kusema ni vyema iwapo kila mtu atachukua jukumu la kuhakikisha kuwa nyama inayoliwa imekaguliwa kikamilifu na sio kungojea hadi pale maradhi yanapozuka, ili kusaidia kupunguza maafa yanayotokea sampuli hii.

Mzee wa kijiji, Charles Korir alisema kuwa wengi waliipata nyama hii kutoka kwa maeneo ya kutengeneza pombe haramu iliyokuwa ikibadilishwa na nyama.

Watu wazima 11 na watoto 6 wamelazwa na wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Olenguruone huku wengine wakiwa walitibiwa na wakaruhusiwa kwenda nyumbani.

Mwili wa mwendazake pia umepelekwa katika makafani ya hospitali hii.

Na Emily Kadzo

 

Leave a Reply