Sunday, April 21, 2024
Home > Counties > Migori > Obado ahofu wageni waweza kuhesabiwa kama wakenya

Obado ahofu wageni waweza kuhesabiwa kama wakenya

Gavana wa Kaunti ya Migori Zachary Okoth Obado,anawataka maafisa wasimamizi wa kusahesabu watu kuhakikisha kuwa raia wa Kenya tu ndio wanahesabiwa.
Alipozungumza na wanahabari katika makao yake rasmi jijini Migori, Gavana huyo alihimiza wakazi kubaki nyumbani mwao wakati shughuli ya kujihesabu inaendelea ili waweze kuhesabiwa kwa sababu shughuli hiyo ni ya manufaa sana katika upangaji na ugawanaji wa rasilimali katika nchi nzima.
“Ukikosa kuwa nyumbani kwako wakati wa kujisajilisha, utasambaratisha hesabu
inayohitajika,” alieleza Obado.
Alieleza kuwa amegundua kuwa hesabu ya wakimbizi kutoka Burundi wanaopitia Migori kwenda katika Makambi ya Kakuma imeongezeka.
Obado alizidi kuwasihi Maafisa Walinda Usalama kuhakikisha kuwa mipaka imelindwa vyema ili kusiwe na visa kama vilivyotokea hapo awali ambapo hesabu ya waliosajiliwa ilikuwa nyingi sana kushinda ya kawaida hasa sehemu ya kaskazini nchini.
Gavana Obado alisema kuwa alipata habari kutoka kwa maafisa wa Msalaba Mwekundu kuwa walikuwa wamepokea wakimbizi ishirini kutoka Burundi na takwimu zao zilionyesha kuwa kila mwezi wao hupokea wakimbizi mia tatu kila mwezi.
Ombi la Gavana huyo ni kuwa wanaopaswa kuhesabiwa katika Kaunti hiyo ya Migori wanafaa kuwa wakazi wa Migori ambao miongoni mwao ni raia wa Kenya wanaoishi katika Kisiwa cha Migingo.
Alionya kuwa uwepo wa watu ambao si raia wa Kenya ni chanzo cha ukosefu wa usalama kwa wakazi.
Obado aidha aliunga mkono viongozi wengine nchini kwa kutaka vijana wasio na ajira peke yao kupewa kazi ya kuwa maafisa wanaoshughulikia usajili wa Wakenya.
Alipinga kitendo cha watu ambao wameajiriwa kupewa nafasi hizo za kazi.
“Kipao mbele kipewe kwa vijana wasioajiriwa kisha cha pili kipewe wakazi wa Migori,” alisisitiza Obado.
Isitoshe, alishikilia kuwa si vijana wote wanapaswa kupewa kazi hizo katika Kaunti ya Migori bali wale wenyeji wa Migori pekee kwa sababu shughuli hii ni shughuli inayofanywa Kenya nzima hivyo basi kila kijana anapaswa kuajiriwa katika Kaunti yake huku akisisitiza kwamba jambo hilo linadhihirisha usawa.
Na Geoffrey Satia/Larissa Ongeri

Leave a Reply