Wednesday, October 9, 2024
Home > Counties > Serikali yaapa kurejesha amani Kitui kusini

Serikali yaapa kurejesha amani Kitui kusini

Serikali imewahakikishia usalama wenyeji wa kaunti ya Kitui wanoishi kwenye mipaka ya kaunti za Kitui na Tana River baada ya wafugaji kutoka kaunti ya Tana River kuvamia mashamba ya wenyeji hao na kuyageuza kuwa malisho ya mifugo yao.

Akizungumza alipozuru maeneo ya Kalambani ambapo inaripotia kuzuka mzozo baina ya jamii hizo mbili mapema wiki hii, kamishena wa kaunti ya Kitui Mbogai Rioba aliandaa mkutano wa amani uliozileta jamii hizo mbili pamoja na kuamuru kila mmoja afuate sheria.

“Nyinyi wafugaji kutoka Tana River mnakosea wenzenu kwa kulisha mifugo katika mashamba yao. Serikali itatumia sheria kuwaondoa hapa kuanzia leo,”akasema Bw Rioba.

Rioba aliwaonya wakaazi kutoka pande zote mbili kukoma kuchukua sheria mikononi mwao huku akitoa onyo kwamba yeyote atakayepatikana na hatia ya kuchukua sheria mkononi mwake atashtakiwa na kupelekwa kortini.

Kulingana na wenyeji wa Kitui kusini, wafugaji hao wanamiliki bunduki haramu na hivyo kuhatarisha maisha ya wenyeji hao.

Wafugaji hao waliohamia maeneo hayo kutokana na hali mbaya ya ukame kaunti ya Tana River walikubali kurudi kwao baada ya serikali kutoa amri na makataa ya kuondoka kwao na kukoma kuharibu mimea katika mashamba ya wenyeji wa Kitui kusini.

Viongozi wa kisiasa waliomba serikali kuu kutafuta suluhu ya kudumu kwani jamii hizi mbili zimekuwa zikizozana tangu mwaka wa 1992.

Maeneo yaliyoadhirika zaidi ni pamoja na lkandani, Kalambani, Syoilovia, Kaatene, Ngaani, Kyamatu na Mutha.

Mwaka jana mzozo kati ya jamii hizo uliathiri shughuli za masomo na kupelekea baadhi ya shule kufungwa na watu kutoroka makwao kutokana na kuhofia usalama wao.

Rioba alikuwa ameandamana na wakuu wa polisi kaunti ya Kitui wakiongozwa na kamanda wa polisi Leah Kithei.

Na Charles Matacho

Leave a Reply