Wednesday, September 18, 2024
Home > Counties > Simba na fisi kuokolewa toka maangamizi

Simba na fisi kuokolewa toka maangamizi

Idadi ya simba na fisi hasa wale wa madoadoa katika mbuga za wanyamapori nchini kenya inatarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo mwaka wa 2030. Hii ni baada ya wizara ya utalii na uhifadhi wa wanyamapori kuzindua mikakati ya kuzuia kuangamizwa kwa wanyama hao.

Akizungumza katika mbuga ya wanyamapori ya Maasai Mara wakati wa kuizndua mpango wa kuwaokoa wanyama pori hao hapo Alhamisi, waziri wa  Utalii na Wanyapori  Najib Balala hakusita kudokeza kuwa serikali i mbioni kuhakikisha maslahi ya simba na fisi wa madoadoa kando na wanyamapori wengine wa dhamana yanatiliwa maanani

Waziri Balala ameongeza kuwa jamii zinazozingira mbuga za wanyamapori zimeazimia kuunga mkono uhifadhi wa wanyamapori na serikali inawapiga jeki.

Waziri  huyo wakati huo huo alikariri msemo wake wa hapo awali wa kuzionya kampuni zote za ki-utalii ambazo zimejenga kambi zisizohalali katika mbuga ya Maasai Mara kwamba chuma chao ki motoni huku akiongeza    kwamba hii imeshusha hadhi ya mbuga hiyo ya kimataifa.

Naye gavana wa kaunti ya Narok Samuel Kuntai Ole Tunai ametilia mkazo kuwa uhifadhi wa wanyamapori hautalemazwa au kukwamizwa na maazimio ya uwekezaji mbugani.

Simba na fisi hawa wa madoadoa katika   mbuga ya Maasai Mara wamekuwa  wakiuwawa kiholela wakiwavamia mifugo na wanadamu hivi kwamba, idadi yao inaanza kupungua mbugani Maasai Mara.

Serikali pia inamaizi madhila ya waathiriwa wa uvamizi wa wanyamapori ambapo kati ya mwaka wa 2014 hadi 2017 shilingi milioni 120 zimetumika kufidia maafa yaliyosababishwa na vuta nikuvute kati ya binadamu na wanyamapori katika kaunti ya Narok. Pia mwezi uliopita shilingi milioni 10.7 zililipwa kwa waliopata majeraha.

Gavana Tunai   kwa upande wake alisema kwamba fisi wa madoadoa ambao  wamekuwa wakiuwawa kiholela  hutekeleza jukumu muhimu katika kusafisha mazingira na kuyafanya kuwa safi kwa kula mizoga ambayo  ingesababisha mradhi kwa  binadamu na wanyama.

Aliongeza  kwamba Mkakati wa Usimamizi wa mbuga ya Maasai Mara hivi karibuni  utasaidia  kuondoa kambi au mijengo isiyo halali katika mbuga hiyo.

“Tutazipiga msasa kambi zote zinazohudumu katika mbuga hiyo ya Maasai Mara na kuziondoa zile ambazo si halali,” Tunai laisema akiongeza kwamba mkakati huo pia utasaidia kuleta uelewano na hata kuhakikisha kwamba watu na wanyama wanaishi pamoja bila mgogoro,” Tunai  aliongeza.

Mbuga ya Maasai Mara inajulikana ulimwengu mzima kwa sababu la tukio la ajabu la kila mwaka ambapo  nyumbu huvuka mto Mara hadi Serengeti katika nchi ya Tanzania na kisha kurudi.Tukio hili hufanyika baina ya mwezi wa Julai na Septemba ambapo watalii wengi huzuru mbuga hii kujionea tukio hili.

Gavana huyo aliiomba serikali kuu kupitia wizara ya Utalii kuendelea kuwatafutia masoko watengenaji bidhaa za ushanga ili kuwaimarisha kiuchumi ambapo alidokeza  kuna makundi kadhaa yamejiunga katika kaunti ya Narok kwa minajili ya kufanya kazi hii na kujipatia mapato.

 

Alisema kuziimarisha jamii zinazoishi karibu na mbuga kiuchumi itasaidi mbuga ya Maaasai mara kuimarika.

 Na Mabel Keya Shikuku

Leave a Reply