Friday, September 22, 2023
Home > Counties > Bungoma > Swala la utovu wa nidhamu katika baadhi ya shule lazua wasiwasi

Swala la utovu wa nidhamu katika baadhi ya shule lazua wasiwasi

Swala la utovu wa nidhamu shuleni limezidi kuwa kitendawili kigumu ambacho jibu lake bado halijapatikana.

          Visa vya utovu wa nidhamu vinazidi kushuhudiwa miongoni mwa wanafunzi katika shule tofauti humu nchini, huku wengi wao wakilalamikia adhabu kali kutoka kwa walimu,kunyimwa muda wa burudani na kuwepo kwa ratiba ya masomo inayobana.

        Jimbo la Bungoma kwa sasa limeathirika pakubwa huku suala hilo likiwa limekita mizizi.

         Katika eneo bunge la kimilili shule mbili za upili za wavulana, Chesamisis na Mtakatifu Luka zililazimika kuwatuma nyumbani wanafunzi baada ya kushuhudiwa kwa migomo ya wanafunzi wiki jana.

        Hapo jana bweni la shule ya upili ya Bukembe iliyo katika kaunti hiyo ya Bungoma liliteketea na kuleta hali ya wasiwasi miongoni mwa walimu wa shule zingine.

          Haya yanajiri siku chache baada ya DCI George kinoti kutoa amri kali kwa wanafunzi watakaopatikana wakikiuka sheria za shule ama kupatikana na kesi zo zote za utovu wa nidhamu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya kwamba watahukumiwa na kuchukuliwa kama watu wazima wanaojua la kufanya, jambo litakaloathiri stakabadhi zao za baadaye wanapotafuta ajira.

          Naye Waziri wa  Elimu prof. George Magoha,juzi akiwa Kajiado aliwaomba wazazi waandae wanao katika hali ya maisha na kuwaamuru walimu kutolegeza kamba katika kutoa adhabu kwa wanafunzi akidai mwanafunzi ye yote hatasazwa ikiwa atapatikana akikiuka  sheria za shule.

           Mkuu was elimu katika Kaunti ya Bungoma Phillip Chirchir amesema uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini haswa cha utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi kwenye shule husika ili kupata suluhu ya kudumu.

          Swali ni je nani anapaswa kulaumiwa katika hali hii inayozidi kuwa donda dugu miongoni mwa shule za upili?ni adhabu ipi ama kiwango kipi cha adhabu anachopaswa kupewa  mwanafunzi kutoka kwa mwalimu?ni hukumu ipi anayopaswa kupewa mwanafunzi atakayepatikana akishiriki katika utovu huo?na mwisho ni mikakati ipi iliyopo ama inayopaswa kuwepo kama njia ya kupigana na hali hii ya utovu wa nidhamu shuleni?

            Ila kutokana na kauli za mkurugenzi wa haki ya jinai na waziri wa elimu ni ishara tosha kwamba serekali ipo tayari kupambana na janga hili.

Aidha ni busara wanafunzi pia kupewa muda wao kujieleza kuhusu mambo wanayopitia shuleni kutoka kwa walimu ikizingatiwa kwamba kuna walimu pia ambao kwa namna moja ama nyingine wanawadhulumu wanafunzi.

Dhuluma wakati mwingine huwafanya wasomi kufanya mambo ambayo si ya kawaida kutokana na kushindwa kuvumilia kwa sababu yakutoskilizwa na walimu na usimamizi wa shule kwa jumla.

na Khaemba Emmanuel/Roseland Lumwamu

Leave a Reply