Tuesday, February 3, 2026
Home > Counties > Wakaazi wa Trans Mara Kusini wapongezwa kwa kudumisha amani

Wakaazi wa Trans Mara Kusini wapongezwa kwa kudumisha amani

Katibu mkuu katika Idara ya Utalii  na Wanyamapori, John Olotuaa amewapongeza wakaazi wa Trans Mara Kusini kwa kudumisha amani akibainisha kuwa maelewano miongoni mwa jamii tofauti tofauti ni muhimu kwa maendeleo endelevu na kuboresha maisha yao pia.

Akizungumza wakati wa shughuli ya ugavi wa chakula katika eneo la Angata Barakoi kwa waathiriwa wa vurugu lililotokea mwezi wa Disemba na kupelekea serikali kuweka agizo la kutotoka nje kwanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa saa kumi na mbili ya asubuhi, amezitaka jamii hizi kuendelea kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama pamoja na kamati za mitaa katika eneo hili ili kuendelea kuimarisha na kudumisha mihimili ya amani.

Aidha, alisema kuwa maafisa wakuu wa usalama wamekuwa wakifuatilia matukio ya eneo hili kwa karibu na kuhusisha uwepo wa amani kutokana na uwajibikaji wa wakaazi na ushirikiano mwema ambao wamekuwa nao na vyombo vya usalama.

Hata hivyo, aliwatahadharisha dhidi ya kuzua vurugu tena akisema kwamba itarudisha nyuma hatua zilizopigwa na serikali ikiwemo masomo ya watoto, matibabu, usafiri na hata huduma zinginezo za muhimu kwa wakaazi.

Baadhi ya bidhaa wakaazi hawa walizozipokea kutoka kwa serikali kuu ni kama vile gunia 600 za mchele, 520 za maharagwe, blanketi 400, sabuni 200, sodo beli 10, magodoro 180.

Naibu Kamishna wa eneo hili, Stephen Emojong, aliwaomba waathiriwa kutofeli kuwapeleka watoto wao wanaopaswa kujiunga na darasa la gredi ya 10 katika shule ya upili akisema kwamba serikali imeweka mikakati kabambe kuona kwamba kila mtoto anafaidika kimasomo.

Emojong aliendelea kusema kuwa serikali imeajiri waalimu wa kutosha, vitabu vimenunuliwa na hata madarasa yalijengwa ili kuona kwamba watoto wanapata mazingira ya elimu ipasavyo.

Familia hizi zilizopata makao ya muda katika shule ya msingi ya Esiteti eneo la Angata Barakoi zimeipongeza serikali kwa kuwakumbuka na kusema kuwa watasalia mstari wa mbele katika juhudi za kudumisha amani ili waweze kuwa mfano mwema katika jamii zingine zilizo na mazoea ya kuvurugana kila mara.

Na Emily Kadzo 

Leave a Reply