Watu wanaoishi na ulemavu wametakiwa kufanyiwa tathmini ya kitaalamu kabla ya kununua au kupewa viti vya magurudumu, kufuatia wasiwasi kwamba matumizi ya vifaa visivyofaa yanasababisha matatizo ya kiafya yanayoweza kuepukika.
Akizungumza wakati wa kongamano la uhamasishaji mjini Narok, balozi wa Bethany Kids, Caroline Wanjera, alionya kuwa matumizi ya aina isiyofaa ya kiti cha magurudumu yanaweza kusababisha changamoto zaidi za kiafya, maumivu ya muda mrefu, na usumbufu katika mwendo.
Wanjera, ambaye anaishi na ulemavu wa uti wa mgongo, alisema ingawa wasamaria wema hutoa msaada wa viti vya magurudumu, mara nyingi hushindwa kushirikisha wataalamu wa afya waliofunzwa kutathmini mahitaji ya mtu binafsi na kupendekeza kifaa kinachofaa.
Alieleza kuwa tathmini hiyo, ambayo pia imeidhinishwa na Baraza la Kitaifa la Watu Wanaoishi na Ulemavu (NCPWD), inahakikisha kuwa mtu mwenye ulemavu anapata kifaa sahihi kulingana na hali yake.
Maoni yake yaliungwa mkono na mkaazi wa eneo hilo, Grace Salantoi, ambaye alitoa wito kwa serikali kuwekeza zaidi katika miundomsingi rafiki kwa watu wanaoishi na ulemavu. Alisisitiza umuhimu wa kurekebisha majengo ya umma ili yaweze kufikika kwa urahisi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Job Mutambai, anayeongoza kikosi cha uhamasishaji, alisema kuwa wasiwasi huo umechochea juhudi za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa tathmini ya kitaalamu kabla ya utoaji wa viti vya magurudumu. Aliongeza kuwa kampeni hiyo inaandaliwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kiti cha Magurudumu Duniani yatakayofanyika Kaunti ya Kakamega tarehe mosi mwezi ujao.
Alisema lengo la kampeni ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa maagizo sahihi ya kitaalamu na kuweka mifumo shirikishi ya msaada kwa watu wanaoishi na ulemavu.
Shirika la Bethany Kids, lenye makao yake Kijabe, limekuwa mstari wa mbele kutetea haki na ustawi wa watu wanaoishi na ulemavu. Tayari limesambaza viti 10 vya magurudumu katika eneo la Narok.
Mpango huo utaendelea katika Kaunti ya Kisii, ambapo viti 50 vya magurudumu vitatolewa, kabla ya kuenea hadi kaunti za Bomet na Kisumu. Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiti cha Magurudumu Duniani, shirika hilo linapanga kusambaza viti 100 zaidi.
Wadau hao pia wamewahimiza wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu kujitokeza kwa wingi katika makongamano ya uhamasishaji, wakisisitiza kuwa watoto hao wanastahili fursa sawa za elimu, kukuza vipaji vyao na kufurahia maisha kama watoto wengine.
Na Emily Kadzo
