Wakaazi wa Olenamara, eneo la Kilgoris, wameiomba Serikali kuingilia kati mzozo wa ardhi unaodaiwa kuchochewa na ugunduzi wa madini ya dhahabu katika eneo hilo, wakisema wamekuwa wakikabiliwa na vitisho na usumbufu kutoka kwa aliyekuwa mwakilishi wa wadi (MCA) wa eneo hilo.
Wakaazi hao walisema hali imekuwa tete tangu kubainika kuwepo kwa madini hayo, huku wakidai kuwa aliyekuwa MCA ameanza kudai sehemu ya ardhi wanayosema imekuwa mikononi mwao kwa muda mrefu.
Wakizungumza baada ya maafisa wa polisi kufika eneo hilo jana asubuhi na kuwakamata watu tisa kufuatia mzozo huo, wakaazi hao walitaka mipaka ya mashamba yanayogombaniwa ithibitishwe rasmi ili kumaliza mvutano unaoendelea.
Daniel Melita, mkazi wa eneo hilo, alisema hawapingi mchakato wa kisheria wa kutatua mzozo huo, lakini wanataka pande zote zihusishwe katika kubaini mipaka halisi ya mashamba yanayogombaniwa.
Alisema baadhi ya wakaazi wanaishi kwa hofu kutokana na madai ya kunyang’anywa sehemu ya mashamba yao, licha ya kusisitiza kuwa wana haki ya kuyamiliki.
Jackson Mbelia, mkazi mwingine, alisema hawajui msingi wa madai kwamba sehemu ya ardhi yao ni ya jirani yao, akitaka maafisa waliohusika na kuweka mipaka hiyo wajitokeze na kutoa maelezo.
Mbelia alisema mzozo huo umewaathiri zaidi wanawake na watoto, wakiwemo baadhi ya wanafunzi ambao walilazimika kutawanyika kutokana na vurugu zilizozuka wakati wa mzozo huo.
“Kuna kilio kikubwa hapa. Tunawaomba viongozi na Serikali wasikie kilio chetu na waje kuchunguza suala hili kwa sababu mambo si mazuri,” alisema.
Narikungera Roikoti alisema wakazi wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara kutokana na mzozo huo, huku familia zikiishi kwa hofu ya kupoteza mashamba yao.
Alitoa wito kwa viongozi wa eneo hilo kuingilia kati haraka kabla mzozo huo haujawa mkubwa zaidi.
“Tunanyang’anywa mashamba yetu na hatujui tutaenda wapi. Tunaomba viongozi wasikie sauti yetu na waje kutusaidia,” alisema.
Susan Kilel alisema wakaazi wanaamini kuwa ardhi hiyo ni yao na wana haki ya kuendelea kuitumia, akitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina na kubaini mipaka halali ya mashamba hayo.
Wakaazi hao walisema wako tayari kushirikiana na Serikali katika kutafuta suluhu ya amani, lakini wakasisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwa wa haki, wazi na kuwahusisha wote wanaodai umiliki wa ardhi hiyo.
Walisema hali hii imeongeza wasiwasi miongoni mwa wakazi, wanaotaka mamlaka kuchukua hatua mapema kuzuia mzozo huo kusababisha madhara zaidi kwa jamii nzima.
Wakaazi hao pia walitaka uchunguzi wa madai ya vitisho na usumbufu ufanyike, wakisema hatua hiyo itasaidia kurejesha utulivu na kuwalinda wanaoishi katika eneo hilo.
Na Emily Kadzo
