Home > Counties > Homa-Bay > Serikali kuendelea kufadhali walemavu shuleni

Serikali kuendelea kufadhali walemavu shuleni

Ni afueni kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Migori baada ya serikali kuu kuwahakikishia kuendelea kwa ufadhili wa masomo yao katika vitengo tofauti.
Akiongea na vyombo vya habari ofisini mwake, kodineta wa Shirika la Wanaoishi na Ulemavu katika kaunti hiyo Bi. July Minyoso alisema kuwa kwa muda sasa, Serikali imekuwa ikifadhili wanafunzi wanaoishi na ulemavu na mpango huo utaendelea kama mojawapo ya mipango ya serikali kuimarisha maisha ya walemavu kote nchini.
Aliongeza kuwa chini ya mpango huo, kila mwanafunzi atapokea kiwango cha asilimia 70 ya karo anayolipa kwa mwaka.
Minyoso aliweka wazi kuwa katika mwaka uliopita wa kifedha 2018-2019, waliweza kulipia wanafunzi thelathini na wanne karo na kuongeza kuwa bado wanapokea maombi ya wanaotaka ufadhili huo katika mwaka wa kifedha wa 2019-2020.
Cha msingi alisema ni lazima anayetuma maombi awe amejisajili kuwa mwanachama wa shirika la wanaoishi na ulemavu nchini (PLWDs) ndipo aweze kupata ufadhili huo.
Alitaja swala la baadhi ya wazazi wanaoishi na watoto walemavu kuwaficha kama changamoto katika juhudi za serikali kujua idadi kamili ya walemavu katika gatuzi hilo na kuwaomba kutofanya hivyo kwani wananyima serikali uwezo wa kuwatengea walemavu pesa za kutosha.
Pia Bi. Minyoso alisema kunao wazazi ambao wanawabagua watoto wao ambao wana ulemavu kwa kutowasomesha wakisingizia kuwa hawana uwezo wa kufanya hivyo ilhali wanasomesha wenzao ambao hawana ulemavu bila kulalamikia kutokuwa na uwezo.
Akizungumzia swala hilo, mwakilishi wa walemavu katika bunge la Migori mheshimiwa Esther Atieno Onana alisema kuwa atawasilisha mswada bungeni kushinikiza mgao zaidi kutoka kwa serikali ya kaunti ya Migori baada ya kugundua kuwa wanachopata walemavu hakitoshi kukidhi mahitaji yao.
Onana alitoa wito kwa walemavu kujitokeza kuhesabiwa kwa wingi baada ripoti kuwa baadhi yao walikua wanataka kususia zoeizi la kuhesabu watu.
Mwakilishi huyo alisisitisa kuwa hesabu ya walemavu kamili ni muhimu kwa sababu itasaidia serikali kuwatengea bajeti yao kulingana na idadi itakayopatikana.
Baadhi walemavu kama vile viziwi walitaka serika kuwaajiri wakalimani kwa lugha ya ishara wakidai hawataelewa yale maafisa wa kuhesabu walitaka kwao.
Hata hivyo alipongeza gavana wa Migori mheshimiwa Zachary Okoth Obado kwa kile alichosema ni kujitolea kwa gavana huyo kufadhili masomo ya baadhi ya wanafunzi walemavu katika kaunti hiyo.
Na Geoffrey Satia/Richard Otieno

Leave a Reply