Tuesday, May 28, 2024
Home > Counties > Wanahabari Kilifi washirikiana kupanda miti kukabiliana na tabia nchi

Wanahabari Kilifi washirikiana kupanda miti kukabiliana na tabia nchi

Huku taifa likitafuta suluhu la mabadiliko ya tabia nchi, kundi moja la waandishi wa habari kutoka kaunti Kilifi limejitosa katika shughli za kupanda miti na uhifadhi wa misitu ili kuchangia kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kundi hilo linalojumuisha wanahabari kutoka vituo mbali mbali humu nchini tayari wamepanda zaidi ya miti 15,000 tangu waanzishe mpango huo wiki chache zilizopita.

Aidha mapema leo kundi hilo  limeshirikiana na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) pamoja na wakaazi wa eneo la Maya na kupanda miti zaidi ya 5000 ili kuhifadhi msitu wa mikoko ulioharibiwa na wakaaazi eneo hilo.

Kulingana na mwenyekiti wa kundi hilo, linalojulikana kama Beyond the Story, Mauren Ongala amesema waliamua kuchukua hatua hio ya kipekee ili kujiunga na jamii katika juhudi za kutafuta suluhu ya mabadiliko ya tabia nchi badala ya kuandika habari bila vitendo.

“Tuliona kwamba kuwa nyanjani na kuandika habari haitufanyi sehemu ya mipango lakini tukitaka kujumuika na jamii na kuwa kati ya ile mikakati ambayo wanafanya kwa maswala ya mazingira ni tuwe nao moja kwa moja,” alisema.

Aidha Ongala alidokeza kwamba kundi hilo lina mipango ya kufanya zoezi la kupanda miti kila mwezi pamoja na kuwahusisha washikadau mbali mbali ili kushirikiana katika kufanikisha azma yao.

Mwandishi wa gazeti la Star Elias Yaa, mwanachama wa kundi hilo, aliongeza kuwa wanampango wa kufuga nyuki katika misitu ya mikoko ili kuwawezesha wakaazi kupata njia mbadala ya kujikimu kimaisha badala kukata miti.

Mratibu wa Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) jimbo la Pwani Maureen Mudi amepongeza juhudi za kundi hilo kwa kuchukua hatua zaidi ya uandishi katika kuhifadhi mazingira.

“Kazi yetu kama Baraza la Vyombo vya Habari ni kuhakikisha tunaihamasisha jamii na pia waandishi wa habari umuhimu wa kuandika kuhusu mazingara na naona nyinyi mnafanya Zaidi ya kuhamasisha. Mnajiunga na jamii kuhakikisha kuwa mazingira yanadumishwa”, alisema.

Aidha Mudi ametoa wito kwa wanahabari nchini kufanya juhudi zaidi ya uandishi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwa kielelezo kwa jamii.

“Hatua hii ni nzuri Zaidi na inafaa ihimizwe kwa waandishi wa habari wote kwa sababu maswala ya tabia nchi ni mazito kwa kila mwandishi wa habari,” alisema.

“Mwandishi akijiunga na jamii kufanya kazi kama hii, kando na kuripoti, anafanya kazi ambayo inasaidia jamii na jamii pia inazidi kujifunza na pia watapata wafadhili ambao watakuja kwa sababu ya kuangaziwa,” Mudi alieleza.

Hatua ya kundi hilo la waandishi inatarajiwa kuchangia katika mpango wa serikali wa kupanda miti milioni 15 pamoja na mikakati mbali mbali ya kuhifadhi mazingira katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Na Jackson Msanzu

Leave a Reply