Home > Agriculture > Watu 12 washikwa na silaha

Watu 12 washikwa na silaha

Maafisa wa usalama katika eneo la Transmara Magharibi katika Kaunti ya Narok wamewatia mbaroni watu 12 kuhusiana na mafarakano mapya ambayo yalizuka baina ya koo mbili za jamii ya Wamaasai katika sehemu hiyo yenye hali tete kiusalama hapo jana.

Akihutubia waandishi wa habari nje ya afisi yake Jumatatu, Kamishna wa kaunti ya Narok, Samuel Kimiti alisema polisi walipata nyuta kumi, mishale 12 na mikuki tatu kutoka kwa washukiwa hao.

Bwana Kimiti alisema washukiwa hao pamoja na wengine waliofanikiwa kutoroka walikuwa wamevamia mkulima mmoja ambaye alikuwa ameenda shambani kuvuna miwa yake Jumapili na hata wakateketekeza shamba hilo la miwa.

Nyumba mbili pia zilichomwa katika mzozo huo baina ya koo za Iruasin-gishu na Siria lakini hakuna alijeruhiwa katika vita hivyo vya jana jioni.

Kamishna huyo pia alisema washukiwa hao watawasilishwa kortini pindi uchunguzi utakapomalizika kujibu mashataka ya uhalifu huo.

Kimiti alionya kwamba huenda wakaongeza masaa ya kuto toka nje katika eneo hilo kama mzozo huo utaendelea.

Masharti ya kutotoka nje baina ya saa kumi jioni na saa moja asubuhi yaliwekwa katika eneo hilo ili kudhibiti vita baina ya koo hizo mbili miezi kadhaa iliyopita.Masharti haya ya kuto toka nje inaenda sako kwa bako na ile ya kitaifa ya Saa tatu usiku hadi saa kumi asubuhi ambayo inaendelea sasa ili kudhibiti maradhi ya Korona nchini.

Kimiti alionya wote wanaochochea uhasama baina ya jamii mbalimbali katika kaunti hii kwamba chuma chao ki motoni.

Kiongozi huyo vilevile alikariri amri yake ya awali kwamba hakuna yeyote atakaye ruhusiwa kulisha mifugo katika misitu katika kaunti hii kwa vile hii imekuwa ikichochea uhasama baina ya jamii mbalimbali.

Kaunti ya Narok hivi karibuni imekumbwa na visa mbalimbali vya vita vya ki-jamii katika kaunti ndogo ya Narok kusini na ile ya kaskazini.

Miezi ya mei na Juni, Watu sita waliuwa katika Olooruasi na Ololoipangi katika eneo hili la Narok kusini na nyumba 15 kuchomwa, ilhali watu wengine wengi wakajeruhiwa katika vita baina ya jamii za kipsigisi na Maasai zinazoishi katika sehemu hiyo baada ya ngombe kuibiwa.

Wiki jana, watu wanne waliuwa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika vita baina ya jamii ya Kipsigis na Maasai katika eneo la Olpusimoru katika kaunti ndogo ya Narok kaskakazini. Vita hivyo vilizuka baada ya vijana wawili kuuwawa wakiwa malishoni katika msitu na watu wasiojulikana na ng`ombe kuibiwa.

Bwana Kimiti amesema leo kwamba utayarishaji wa stakabadhi zao za kumiliki ardhi zao u karibu kumalizika ili kujaribu kumaliza mzozo huu.

Usalama pia umeimarishwa katika eneo hilo.

Na  Mabel Keya-Shikuku

Leave a Reply