Wednesday, February 11, 2026
Home > Counties > Vijana waombwa kujisajili kama wapiga kura

Vijana waombwa kujisajili kama wapiga kura

Gavana wa gatuzi la Narok, Patrick Ole Ntutu amewaomba vijana ambao hawajajiandikisha kama wapiga kura kuwajibika na kuhakikisha hawawachwi nyuma katika kufanya maamuzi yao ya kuchagua kiongozi bora katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwaka wa ujao.

Akiongea na wakaazi wa eneo la Mulot lililoko katika gatuzi dogo la Narok Kusini, wakati wa sherehe ya kustaafu kwa kasisi Samuel Mosonik wa kanisa la AGC Mulot, Ntutu alisema kuwa kuwa kujiandikisha kama mpiga kura kuna mpa mtu uwezo wa kufanya maamuzi ya busara kuhusu aina ya uongozi utakaoifanya nchi kusonga mbele.

Ntutu alisema kuwa iwapo vijana wetu ndio kesho yetu kama inavyoaminika, basi itakuwa vyema kwao kuweka sauti yao katika maamuzi makuu katika nchi hii, kuwajibika ili tupate aina maendeleo na kujenga taifa lililo imara.

Aidha, aliwaomba vijana kutotumika vibaya na wanasiasa katika kuzua vurugu au kuzuia wawaniaji wengine kutouza sera zao kwa wakaazi wakati wa kampeni akisema kuwa hali hii huzua vurugu na kuleta uhasama kati ya jamii zilizokuwa zikiishi kwa amani.

Aliomba wote kusalia na utulivu na kuwa mabalozi wa amani kabla na ahata baada ya uchaguzi.

Kulingana na tume huru ya uchaguzi na mipaka ya IEBC, vijana wanawakilisha asilimia 70 ya idadi ya watu nchini ilhali ni asilimia 40 pekee waliojitokeza katika kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022; hali inayoonyesha ni wengi waliosalia nyuma katika kuchagua viongozi wanaofaa kuendeleza maendeleo.

Hata hivyo, serikali imejaribu kuweka mikakati kabambe kuona kwamba wengi hasa vijana wanajiandikisha kama wapiga kura katika uchaguzi mkuu ujao kama vile kurahisisha mchakato wa kupata kitambulisho ambacho ni stakabadhi muhimu wakati mtu anapojiandikisha, matangazo katika vyombo vya habari n ahata kuwepo kwa baraza vijijini kuwaelezea wakaazi umuhimu wa kuwa na kitambulisho n ahata kupiga kura.

Na Emily Kadzo

Leave a Reply