Home > Editor Picks > Wataalamu wajadili nafasi ya Kiswahili katika teknolojia na maendeleo

Wataalamu wajadili nafasi ya Kiswahili katika teknolojia na maendeleo

Wataalamu wa lugha ya Kiswahili kutoka mataifa mbalimbali wamekutana katika Chuo Kikuu cha Kisii kujadili nafasi ya lugha hiyo katika maendeleo, wakisisitiza umuhimu wake katika teknolojia, utafiti na utengenezaji wa maudhui ya kidijitali yanayoakisi tamaduni za Afrika Mashariki.

Kongamano hilo la Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) limewaleta pamoja zaidi ya washiriki mia mbili kutoka Kenya, Tanzania Bara na Zanzibar, Rwanda, Burundi pamoja na wataalamu kutoka vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya.

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Elimu wa Gatuzi la Mombasa, Dkt. Mbwarali Kame, alisema lugha ya Kiswahili iko na nafasi muhimu katika mifumo ya kidijitali.

“Ni wajibu wetu kama Waafrika kuienzi lugha ya Kiswahili ili iweze kutambulika zaidi kimataifa na kuchangia maendeleo ya teknolojia,” alisema Dkt. Kame.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Chacha Nyaigotti Chacha alisisitiza kuwa Kiswahili kina uwezo wa kutumika kikamilifu katika nyanja za elimu, sayansi na teknolojia bila vikwazo vya msamiati.

“Lugha yoyote hukua kupitia matumizi. Kiswahili kina msamiati na istilahi za kutosha, na pale ambapo hazipo, tuna uwezo wa kubuni na kujiendeleza,” alisema Profesa Chacha.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki, Dkt. Caroline Asiimwe, alitoa wito wa kuimarishwa kwa uwekezaji katika utafiti na mifumo ya akiliunde (AI), akisisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa data za pamoja katika ukanda huo.

“Kuna haja ya kuwa na data ya pamoja ya Kiswahili itakayosaidia kukuza matumizi yake katika teknolojia na ubunifu,” alisema Dkt. Asiimwe.

Naye Dkt. Shadidi Ndosa kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s, Tanzania, aliangazia umuhimu wa Kiswahili katika utengenezaji wa maudhui ya watoto yanayozingatia tamaduni za Kiafrika.

“Ni muhimu kuhakikisha maudhui ya watoto yanayoandaliwa kwa Kiswahili yanaakisi mila, desturi na utu wa Afrika Mashariki badala ya kuiga tu yale ya nje,” alisema Dkt. Ndosa.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuunda maudhui kama katuni, vitabu na bidhaa nyingine za kidijitali zinazokuza utamaduni wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Profesa Clara Momanyi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta alisema kuna haja ya kuhakikisha Kiswahili hakiwi nyuma katika kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.

“Tunapaswa kushirikiana na wataalamu wa teknolojia ya lugha ili kuhakikisha Kiswahili kinaingia kikamilifu katika matumizi ya kiteknolojia kama zilivyo lugha nyingine za kimataifa,” alisema Dkt. Momanyi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAKAMA, Dkt. Juliet Jagero, aliwataka wataalamu wa Kiswahili kutoa mwelekeo madhubuti wa namna lugha hiyo itakavyoingizwa katika teknolojia, badala ya kuiga mifumo kutoka nje bila muktadha wa lugha hiyo.

Alisema kongamano hilo linalenga kutoa maazimio yanayosaidia kuongeza sera na mikakati ya kuendeleza Kiswahili, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi cha sasa wanaotumia teknolojia kwa kiwango kikubwa.

“Kiswahili kipo wapi katika ulimwengu wa teknolojia? Hili ndilo swali tunalotaka kulijibu kupitia mjadala huu,” alisema Dkt. Jagero.

Washiriki walikubaliana kuwa Kiswahili ni lugha yenye uwezo mkubwa wa kuwa chombo cha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia, iwapo kitaendelezwa kupitia tafiti, sera thabiti na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Na Misheba Alfred na Mercy Osongo

Leave a Reply