Home > Agriculture > Kiongozi apigia upato kwa kilimo cha mpunga

Kiongozi apigia upato kwa kilimo cha mpunga

Mjumbe wa Bunge la Kaunti ya Homa Bay ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika kilimo cha mpunga ili kuimarisha utoshelezi wa chakula na kuunda nafasi zaidi za ajira katika kaunti hiyo.

Akizungumza katika bunge la kaunti, mwakilishi huyu wa Wadi ya Kagan, David Hamilton alisema kuwa kaunti hiyo ina uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa mpunga kupitia mpango wa unyunyuziaji maji wa Oluch Kimira, ulioko katika Wadi ya Kagan na maeneo jirani.

“Tuna uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa mpunga kupitia mradi wa maji wa Oluch Kimira. Tukiongeza uwekezaji katika sekta hii, tutaimarisha utoshelezi wa chakula na kuunda nafasi nyingi zaidi za ajira kwa wakazi wetu,” alisema Hamilton.

Alieleza kuwa licha ya uwepo wa mpango huo wa umwagiliaji maji, maendeleo katika upanuzi wa kilimo cha mpunga yamekuwa ya kiwango cha chini, hali ambayo imewaathiri wakulima pamoja na wadau wengine wanaotegemea zao hilo kama chanzo cha mapato.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba bado hatujatumia kikamilifu uwezo uliopo. Wakulima wengi wanaendelea kukumbwa na changamoto za uzalishaji mdogo, jambo linaloathiri mapato yao na uchumi wa eneo hili,” aliongeza.

Hamilton alipendekeza kuongezwa kwa eneo la ardhi linalotumika kulima mpunga ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo.

“Kuongeza eneo la kilimo cha mpunga hakutanufaisha wakulima pekee bali pia sekta ya usafiri, wafanyabiashara na wadau wengine wanaotegemea shughuli zinazohusiana na zao hili,” alisema.

Mwakilishi huyo wa Wadi pia alieleza wasiwasi wake kuhusu kufungwa kwa baadhi ya viwanda vya kusaga mpunga kutokana na upungufu wa malighafi.

“Baadhi ya viwanda vya kusaga mpunga vimelazimika kufunga shughuli zake kwa sababu ya ukosefu wa malighafi ya kutosha. Hii imeathiri biashara na kusababisha kupotea kwa nafasi za ajira katika kaunti yetu,” alisema.

Hamilton alibainisha kuwa viongozi na wadau mbalimbali wameandaa sera za kusaidia sekta ya mpunga, lakini akasisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati mingine itakayochangia ukuaji endelevu wa sekta hiyo.

Aidha, alisema kuwa Homa Bay imejifunza kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika Kaunti ya Kirinyaga kupitia mradi unyunyuziaji maji wa Mwea.

“Tunataka kuiga mifano iliyofanikiwa kama Mwea, ambapo sera madhubuti zimewasaidia wakulima wa mpunga kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao. Tunaamini Homa Bay inaweza kufikia mafanikio kama hayo,” alisema.

Hamilton alisisitiza kuwa kuongezwa kwa eneo la kilimo cha mpunga kutaboresha upatikanaji wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kaunti.

“Kufufuliwa kwa sekta ya mpunga kutachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Homa Bay na kuboresha maisha ya wananchi wengi kupitia ajira na ongezeko la mapato,” alisema.

na Regina Joy na Sitna Omar

Leave a Reply