Monday, September 25, 2023
Home > Counties > Elgeyo Marakwet > KWS kumsaka simba

KWS kumsaka simba

Shirika la Wanyama Pori nchini (KWS) limewahakikishia wakazi wa eneo la Moiben kaunti ya Uasin Gishu kwamba linafanya kila juhudi kuona kwamba simba aliehamia eneo hilo kutoka kaunti ya Laikipia amekamatwa.

Afisa anayesimamia shirika hilo, John Ngalia alisema tayari amewasiliana na kitengo cha afya ya wanyama na kile cha ndege akisema kwamba maafisa wa vitengo hivyo wanasubiri kubadilika kwa hali ya anga.

Ngalia aliwasihi wakazi wa eneo hilo wasimdhuru simba huyo wa kiume akisema simba ni mojawapo wa wanyama pori ambao wamo hatarini ya kutoweka kwani idadi yao inaendelea kupungua kwa kasi.

“Ni muhimu tuweze kuwachunga wanyama hawa kutokana na mchango wao katika sekta ya utalii ambayo huchangia pakubwa uchumi wa nchi,” alisema Ngalia.

Kulingana na Ngalia, mnyama huyo tayari amewaua ng’ombe wawili mmoja alhamisi na mwingine jumamosi wiki jana jambo ambalo huenda likawaghadhabisha wakazi.

Afisa huyo alisema nyayo za simba huyo zilionekana karibu na shamba la mkulima mmoja mashuhuri anayejulikana kama Kruger akiongeza kuwa anajaribu kuingia ndani lakini anazuiwa na ua la stima linalozunguka shamba hilo.

Akisema mnyama huyo hutembea usiku, Ngalia aliwashauri wakazi kutotembea usiku akiongeza kuwa ikiwa ameshiba huwa mtulivu na hawezi kumvamia mtu kama hajachokozwa.

Na  Alice  Wanjiru

Leave a Reply