Kamanda wa polisi wa gatuzi dogo la Narok Kusini, Stephen Mwoni amewataka wanandoa na familia kutatua mizozo ya uhusiano kwa amani ili kuepukana na visa vya kusikitisha vinavyohatarisha maisha ya wasio na hatia na kuharibu mali.
Hisia za Mwoni zinakuja baada ya mwanamume mmoja kudaiwa kuchoma zaidi ya nyumba saba za kupangisha za mbao katika Kituo cha Biashara cha Kimogoro eneo la Amalo, kufuatia kutoelewana na mpenzi wake ambaye inasemekana alikuwa akiishi katika mojawapo ya nyumba hizo.
Polisi wameanzisha msako wa kumtafuta mshukiwa anayeaminika kutoroka baada ya tukio hilo.
Tukio hili lilizua wasiwasi mwingi kwa wapangaji na kupelekea wengi kukimbilia usalama huku miale ya moto ikienea kwa kasi katika majengo hayo.
Wakaazi waliouona moto huo walikimbilia eneo la tukio kujaribu kuudhibiti kabla haujasambaa katika nyumba zaidi na maeneo ya biashara.
Mmiliki wa nyumba hizo, Jeremiah Kirui, alimshukuru Mungu kwamba hakuna mtu aliyepoteza maisha licha ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto huo.
“Tunashukuru kwamba watu wanaoishi katika nyumba hizo walifanikiwa kutoroka na kuokoa maisha yao. Lazima tuwe waangalifu kuhusu wale tunaowaruhusu kuishi katika nyumba zetu,” alisema Kirui.
Kakake, Dominic Kirui, alitoa wito wa kuhakikiwa zaidi kwa wapangaji ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.
“Mtu anapokuja nyumbani kwako kukodisha, unapaswa kumchunguza na kupata hati zake za utambulisho ili kufuatilia iwapo kutakuwepo na tukio la kuhatarisha maisha ya wapangaji wengine,” alisema.
Maafisa wa polisi waliungana na wakaazi kukabiliana na moto huo, na kusaidia kuuzima.
Mwoni aliwahakikishia wakaazi kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini na kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo.
“Tunashuku kuwa moto huu ulianzishwa kwa makusudi na mtu, suala hilo lipo katika uchunguzi na kila kitu kitafanyika kwa weledi na atakayepatikana na hatia atafikishwa mahakamani,” alibainisha Mwoni.
Mwoni aliwataka wananchi kuwa waangalifu na kuripoti mara moja matukio ya moto na shughuli zinazotiliwa shaka na kuhatarisha maisha ya wakaazi.
“Kuweni waangalifu sana na mtoe taarifa mara moja mnapoona matukio ya moto yanayotokea katika nyumba za kupanga, majengo ya biashara au nyumba, hasa katika kituo cha polisi kilichoko karibu,” alisema.
Tukio hilo limezua wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa visa vya mizozo ya kinyumbani kuzidi kwani vinaweka jamii nzima hatarini na ni sharti watu wakumbatie kuishi kwa umoja.
Na Hillary Shimnagha and Emily Kadzo
