Mgombeaji wa kiti cha ubunge wa gatuzi dogo la Emurua Dikirr katika Kaunti ya Narok kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA), David Keter almaarufu kama Dollarline, ametangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika jana.
Dollarline aliibuka mshindi baada ya kupata kura 18,266 katika uchaguzi huo uliowashirikisha wagombeaji watano. Mpinzani wake wa karibu Vincent Kibet wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) alipata kura 10,760 na kushika nafasi ya pili.
Mgombeaji wa chama cha National Vision Party (NVP), Gideon Koech, alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 190. Cherono Desma wa chama cha PNU alipata kura 80 huku Kiprono Rotich wa chama cha RLP akifunga orodha kwa kura 62.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Mogondo, msimamizi wa uchaguzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Caleb Gekonde, aliwashukuru wakazi wa Emurua Dikirr kwa kudumisha amani wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Gekonde alisema uchaguzi huo ulikuwa wa huru, haki na uliofanyika kwa uwazi bila visa vikubwa vya vurugu au hitilafu zilizoweza kuathiri matokeo.
Aidha alisema jumla ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo zilikuwa 29,538 kati ya wapigakura 44,343 waliosajiliwa katika eneo hilo, hali inayotafsiriwa kuwa asilimia 66.6 ya wapigakura walijitokeza kushiriki uchaguzi huo.
Aliongeza kuwa kura 180 ziliharibiwa kutokana na kuwekwa alama kimakosa na hivyo kutohesabiwa katika kura halali.
Baada ya kutangazwa mshindi, Dollarline aliwashukuru wakazi wa Emurua Dikirr kwa kumpa nafasi ya kuwaongoza na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na wananchi ili kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.
“Kwanza namshukuru Mungu na wananchi wa Emurua Dikirr kwa kuonyesha imani kubwa kwangu. Nitafanya kazi kwa bidii kuhakikisha ahadi nilizotoa wakati wa kampeni zinatimizwa,” alisema.
Pia aliwataka wakazi kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili kusaidia kuleta maendeleo zaidi katika gatuzi hilo.
Uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr ulifanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Johanna Ng’eno, aliyefariki katika ajali ya helikopta iliyotokea eneo la Mosop, Kaunti ya Nandi, mwezi Februari mwaka huu.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na mwanahabari Nick Kosgei, afisa wa Huduma ya Misitu nchini (KFS) Amos Kipngetich, mwalimu Carlos Keter, mfanyakazi wa serikali ya Kaunti ya Narok Wycliffe Rono na rubani George Were.
Na Emily Kadzo & Hillary Shimnagha
